TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM, Mtanzania
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Bara Tundu Lissu anatarajiwa kuwasili nchini leo na atahudhuria mazishi ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.
Lissu amekaa nje ya nchi miaka mitatu sasa baada ya kuondoka kwa shambulio la risasi lililotokea mjini Dodoma ,Septemba 7, mwaka 2017, saa 7 mchana, Area ‘D’, kwenye nyumba ya makazi ya viongozi wa Serikali mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila ilieza kuwa baada ya kutokea shambulizi hilo, Lissu alipata matibabu ya awali hapa nchini na baada kusafirishwa kwa ndege ya wagonjwa hadi Nairobi kwa matibabu.
“Lissu kwa sasa anatimiza mwaka wa tatu na anarejea hapa nchini baada ya kupona kikamilifu. Natumia fursa hii kuwaalika watanzania na wanachama wa Chadema kuwa waje tukutane uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), kwa lengo la kumpokea makamu mwenyekiti wa chama Lissu,”alisema Kigaila.
Alisema sababu kuwa ya kwenda kumpokea kiongozi wao huyo ni aliondoka nchini kwenda Ubelgiji kwa matibabu na si kwa utalii au kutafuta kazi.
“Lissu amekaa nje ya nchi kwa miaka mitatu akiuguza majeraha ambayo hakupata ajali ya gari, hakuanguka juu ya mti akicheza bali aliyapata kwa kupigwa risasi na watu ambao hadi leo wanasemekana wasiojulikana,”alisema.
Alisema kiongozi huyo alipigwa risasi kwa namna ambayo haikuwahi kutokea katika historia ya nchi na wanakwenda kumpokea kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kumponya kwakuwa hakuna aliyetegemea kama angerejea akiwa hai.
“Anarejea nchini akiwa na akili zake timamu akitembea kwa miguu yake miwili kwakuwa alivyoondoka siku ile hakuna aliyetegemea ndani ya saa mbili atakuwa hai kwani mwili wake ulikuwa umetobolewa matundu na kufumuliwa vibaya,”alisema.
Aliongeza kuwa yeye binafsi ni kati ya watu wachache walioshuhudia matundu ya risasi eneo la tukio ambapo walishuhudia matundu 38 ya risasi hizo yakiwa yametoboa gari.
Alisema risasi 16 ndizo zilikutwa mwilini mwa Lissu na ziliondolewa na madaktari waliokuwa wakimpa tiba mbali ya zile zilizokuwa zimetoboa mwili na kutoka.
“Waliompiga walitaraji kusikia matangazo ya kifo baada ya saa chache lakini kwa uwezo wa Mungu ashukuriwe anarejea akiwa hai,’’ alisema Kigaila.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake