Sunday, July 19, 2020

VIASHIRIA VYA KUJUA KAMA UNAPENDWA


UPO kwenye uhusiano wa kimapenzi? Unahisi unapendwa na mpenzi wako? Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza.

Kwenye uhusiano, si wote hupenda kuelewa mpenzi wake anampenda kiasi gani. Pengine saa nyingine hata kutamani angekuwa na uwezo wa kuona nafsi ya mpenzi wake huyo ni kwa kiasi gani penzi lao ni imara; bahati mbaya au nzuri, haiwezekani!

Hata hivyo, kuna dalili zinazoonekana baina ya wapenzi ambazo huashiria endapo mpenzi wako huyo anakupenda au la.

Hii huambatana na kutokana na tabia na nyendo za mpenzi wako huyo dhidi yako.

Baadhi ya viashiria ambavyo vinaweza kukusaidia katika kutafakari au kutambua endapo mpenzi wako huyo ni kweli anakupenda, ni hivi vifuatavyo;

Mawasiliano kati yenu; hapa unaangalia mawasiliano yenu kwa njia ya simu na vifaa vingine. Sasa hivi mawasiliano yamerahisishwa mno kama vile kupiga simu, njia za meseji kama WhatsApp, Viber, Skype na SMS. Kwa yeyote aliye na simu ya mkononi, ni rahisi kuwasiliana na mpenzi wake wakati wowote ule. Mawasiliano ni njia mojawapo muhimu mno katika kujenga na kuboresha mawasiliano kati ya wapenzi.

Inapotokea mawasiliano hayo yameelemea zaidi upande mmoja siku zote; hapa kuna tatizo. Kimsingi mawasiliano hupaswa kuwiana (mtu na mpenzi wake, wote watafutane kwa usawa) ingawa inaweza kupishana kidogo kutokana na sababu mbalimbali.

Ukiona hakutafuti siku zote hadi uanze wewe au anakukatia simu na kukuzimia bila maelezo yoyote ya msingi, kuwa mkali kila ukimtafuta, kukuonesha kana kwamba simu zako kwake ni kero, basi ujue wewe ni kero kwako na hakuna mapenzi hapo.

Ushirikiano kati yenu; hapa wapenzi wanapaswa kushirikiana kwenye masuala yale ambayo ni ya msingi kwenye maisha. Kila mmoja anapaswa kushiriki na kujitoa kwa mpenzi wake kwa yale yote ambayo huitaji ushiriki kwa mpenziwe. Ushirikiano huu upo wa aina mbili; kuna ushirikiano wa hali ambao huu ni namna ambavyo wewe na mpenzi wako hushirikiana hasa kwenye mambo ya kijamii, kifamilia na kadhalika.

Ikiwa pale unapokuwa na tatizo kama vile kuugua au kuuguliwa, misiba au matatizo mengine yoyote, yeye siku zote ana sababu za kushindwa kuwa karibu yako. Na ikitokea akapata nafasi yupo juujuu akionesha dalili za kutokuwa na wewe, basi ujue hakupendi.

Pia kuna ushirikiano wa mali; hapa unaangalia namna ambavyo wewe na mpenzi wako hushirikiana linapokuja suala la kujitoa kwa vitu vihusuvyo pesa bila kujali kipato cha mwenzako. Ikiwa una mpenzi wako akawa na shida ama kuhitaji msaada wa kifedha au unaohusisha matumizi ya fedha (bila kujali ni mwanamke au mwanaume), huwa ni muhimu kutoa msaada huo.

Taratibu za kuonana; hapa mtu yeyote hata kama akiwa na majukumu kiasi gani, akimpenda mwenziye (iwe kwa mwanamke au mwanaume), atatafuta tu muda kwa ajili ya kuwa na mpenzi wake. Haijalishi huo muda utakuwa mfupi au mrefu, dakika chache au saa, ila tu lile wazo la kutomuona mpenzi wake kwa muda mrefu na hali yupo karibu na ana uwezo huo, linamkosesha raha.

Ikiwa mpenzi wako yupo karibu na unajua fika ana uwezo wa kukuona na kuwa na wewe mara kwa mara lakini haipo hivyo, ni moja ya dalili ya kutopendwa na huyo mtu (labda kuwe na sababu za msingi na iwe ni kitu cha kupita na si tabia yake).

Kwa leo naishia hapa tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine moto, nakutakia wikiendi njema.

Mahaba
Xclusive
Hashim Aziz
+255 719401968
GPL

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake