ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, July 11, 2020
WAAMUZI SITA SIMBA, YANGA HADHARANI
WINFRIDA MTOI – DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la SokaTanzania (TFF), limetaja majina ya waamuzi sita watakaochezesha mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho maarufu Kombe la Azam utakaopigwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi hao ni Abubakar Mturo kutoka Mtwara atakayesimama kati, wasaidizi wake ni Abdallah Mwinyimkuu(Singida), Nadeem Aloyce, Ramadhani Kayoko, Frank Komba na Kassim Mpanga(Dar es Salaam), wakati kamishina wa mchezo ni Ally Katolila.
Katika hatua nyingine
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imetaja idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuingia kwenye mchezo huo kuwa ni 30,000 badala ya 57, 000 ambayo ni uwezo wa Uwanja wa Taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuph Singo, alisema hatua hiyo inalengo la kuchukua tahadhari ili kuepuka maambukizi ya virusi hatari vya ugonjwa wa corona.
“Bado hatujapewa taarifa kama ugonjwa wa corona umekwisha nchini hivyo lazima tuendelee kuchukua tahadahari katika kujikinga, katika hilo leo(jana) wizara tumekutana na viongozi wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) pamoja na wale wa timu hizo ili kujadili mambo mablimbali, ikiwemo idadi ya watazamaji watakaoruhusiwa kuingia uwanjani.
“Kutokana na makubaliano ya pande zote, tiketi zitauzwa kulingana na idadi iliyotolewa huku wale watakaokosa tiketi wakitakiwa kubaki majumbani kufuatilia kupitia luninga,”alisema Simgo.
Singo aliongeza : “Shabiki atakayepata tiketi ya kuingia uwanjani lazima afuate taratibu za afya zilizowekwa ambazo ni kuvaa barakoa wakati wa kwenda uwanjani, kunawa mikono kwa maji tiririka na kukaa kwa umbali wa mita moja.”
Simba yatamba kuiliza Yanga
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara ametamba kuwa watawachapa watani wao Yanga na kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja huo Machi 8, mwaka huu.
“Msimu huu tumeteseka sana hadi inafikia hatua wanafanya ‘birthday’ kila tarehe nane, hii imetuumiza Wanasimba kwa sababu sisi ndiyo tulikuwa na kikosi bora,” alisema Manara.
Alitaka kilichosababisha kupoteza mchezo wa Machi 8 kuwa ni kutokana na kikosi chao kuingia kukamia kuwa na morali ya juu, walipambana na kuingia uwanjani wakiwa wamekamia.
“Lakini kipindi hiki hatutakubali kufungwa na Yanga, unadhani ukipoteza tena mechi hii utawaambia nini Wanasimba, hawatatuelewa kabisa na raha ya ubingwa itakuwa haipo,” alifichua Manara.
Alifichua kuwa hata mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo uliomalizika kwa suluhu walichezesha kikosi chenye mchanganyiko ili kutunza silaha za kuwaadhibu watani wao.
Manara alitamba kuwa mchezo huo wanauchukulia kama kwenda kukamilisha ratiba ya kujiandaa na fainali za michuano hiyo itakayopigwa mjini Sumbawanga.
“Tumeshamaliza mechi ya nusu fainali, mashabiki wetu wa Simba wa Sumbawanga na mikoa ya jirani wajiandae kupokea timu yao, tunakuja kucheza fainali huko,” alitamba
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment