Thursday, August 6, 2020

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU ZOEZI LA UTOAJI FOMU KWA WAGOMBEA WA KITI CHA RAIS


Dailynews
Tume ya Taifa ya Uchaguzi leo jumatano tarehe 05 Agosti, 2020, imeanza kutoa fomu kwa Wagombea wa Kiti cha Rais katika Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.

Katika siku ya kwanza ya zoezi hili, jumla ya Wagombea watatu wamechukua fomu za kugombea Kiti cha Rais katika ofisi za Tume zilizopo Njedengwa jijini Dodoma. Wagombea waliochukua fomu ni Bw. Seif Maalim Seif wa chama cha Alliance for African Farmers Party (AAFP), aliyeambatana na Mgombea Mwenza Bw. Rashid Ligania Rai. Wagombea wengine ni Bw. Philipo John Fumbo wa Chama cha Democratic Party (DP) na Bw. Leopold Lucas Mahona wa Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA) aliyeambatana na Mgombea Mwenza Bw. Hamis Alli Hassan.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kukabidhi fomu hizo kwa Wagombea hao, Mwenyekiti wa Tume Jaji wa Rufaa (Mst) Mhe. Semistocles Kaijage amesema siku ya Uteuzi Wagombea watarejesha fomu hizo na baada ya kujiridhisha kuwa wanazo sifa itawateua.

“Itakapofika siku ya Uteuzi tarehe 25 Agosti, 2020 mtarejesha fomu zenu hapa Tume, na Tume baada ya kujiridhisha kuwa mnazo sifa itafanya uteuzi”

Aidha Jaji Kaijage amewapongeza Wagombea hao kwa hatua ya kuteuliwa na vyama vyao kuwa Wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais kupitia vyama vyao vya Siasa.

“Ninawapongeza kwa kutumia haki yenu ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa. Ushiriki wenu utachangia kudumisha demokrasia nchini mwetu na ninawatakia kila la heri” amesema Mhe. Kaijage

Mapema akimkaribisha Mwenyekiti wa Tume kukabidhi fomu kwa Wagombea, Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera Charles aliwaeleza Wagombea utaratibu unaopaswa kufuatwa katika mchakato huo ikiwa ni pamoja na kuzingatia sifa za Wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, udhamini wa Mgombea, fedha za dhamana na kusaini tamko la kuheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi.

“Tutawapatia nakala ya kijitabu cha Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, tunawasihi mkisome na kuzingatia maadili wakati wote wa kipindi cha kampeni”

Kwa mujibu wa ratiba ya Uchaguzi Mkuu, zoezi la utoaji fomu kwa Wagombea wa kiti cha Rais litafanyika kuanzia tarehe 5 hadi 25 Agosti, 2020.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake