Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na watumishi wa Idara ya Afya Halmashauri ya Chemba wakati alipofanya ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo mkoani Dodoma kwa lengo la kufanya ukaguzi wa maendeleo ya miundombinu bora ya vyoo kwenye Halmashauri hiyo inayotekeleza mpango maalumu wa usafi wa mazingira (Water, Sanitation and Hygiene, WASH). Muonekano wa Baadhi ya Majengo ya Hospitali ya Halmashauri ya Chemba iliyoko mkoani Dodoma yakiwa mbioni kukamilika
Wajumbe wa Kamati ya kituo na baadhi ya Watumishi wa Kituo cha Afya Hamai kilichopo Halmashauri ya Chemba wakimfatilia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima (HAYUPO PICHANI) wakati alipotembelea Kituo hicho kilichpo mkoani Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Kituo cha Afya Hamai kilichopo Halmashauri ya Chemba wakimfatilia Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima (HAYUPO PICHANI) wakati alipotembelea Kituo hicho kilichpo mkoani Dodoma.
Na. Majid Abdulkarim, Chemba
Serikali imewataka Wataalamu wa Afya Nchini kutekeleza majukumu yao kwa ubunifu katika kubaini na kutumia fursa zinazowazunguka ili kuongeza kasi ya kutatua changamoto za kiafya zinazoikabili jamii wanayoitumikia badala ya kufanya kazi kwa mazoea ya kusubiri maelekezo toka wizarani.
Wito huo umetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotembelea Kituo cha Afya Hamai kilichopo Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma kwa lengo la kufanya ukaguzi wa maendeleo ya miundombinu bora ya vyoo kwenye Halmashauri hiyo inayotekeleza mpango maalumu wa usafi wa mazingira (Water, Sanitation and Hygiene, WASH).
Katika ziara hiyo Dkt. Gwajima alipata taarifa inayoonesha takwimu za hali ya miundombinu ya vyoo kuwa asilimia 23 ya kaya ndiyo zenye vyoo bora na asilimia 20 ya kaya hawana vyoo kabisa na kaya zilizobakia zina vyoo vinavyohitaji kuboreshwa.
Kufuatia takwimu hizo Dkt. Gwajima amesema kuwa wataalamu na jamii kwa ujumla wanawajibu wa kutambua kuwa choo bora ni msingi wa ustawi wa uchumi katika kaya na taifa kwa ujumla kwani wananchi wengi zaidi wakiweza kuepuka kuugua magonjwa ya kuambukiza yanayosababishwa na ukosefu wa vyoo bora wataepuka kutumia muda na fedha kwenda kutibiwa na fedha hizo ngazi ya kaya au taifa zitaelekezwa kwenye shughuli za maendeleo na muda wa kutafuta matibabu utaelekezwa kwenye uzalishaji mali na maendeleo kwa ujumla hivyo kukuza uchumi wa kaya na taifa.
Aidha Dkt. Gwajima amezitaka Timu za Afya za Halmashauri kuzijengea uwezo Kamati zinazosimamia Vituo vya Afya ili wajumbe wake wawe na uelewa mpana zaidi juu ya umuhimu wa kila Kaya kuwa na choo bora kwa kutumia lugha nyepesi zaidi katika kufikisha ujumbe kwa wananchi juu ya madhara ya nyumba au kaya kutokuwa na choo bora ili jamii yenyewe ione umuhimu wa kuchukua hatua za kuhamasisha na kutekeleza bila shurti.
“Ni imani yangu kuwa jamii wakipata elimu sahihi kwa lugha nyepesi na inayoonesha uhusiano wa ukosefu wa vyoo bora na afya za wanajamii na athari za kiuchumi ngazi ya kaya na taifa kwa ujumla wananchi wenyewe wataimiliki hii ajenda bila shurti na watahamasika kujenga vyoo bora kwa kuhamasishana wao wenyewe katika maeneo wanayoishi”, ameeleza Dkt. Gwajima
Lakini pia Dkt. Gwajima ametoa rai kwa watendaji wa afya kuwa wanatakiwa kuwa wabunifu katika kutatua kero mbalimbali za wananchi kwa kuwashirikisha waweze kubaini fursa zilizopo na kuacha tabia ya kuingia kazini na mtazamo wa kusubiri maelekezo toka ngazi ya juu wakati changamoto zingine ufumbuzi wake uko ndani ya uwezo wao kwa kushirikiana na jamii wanayoihudumia.
“Tanzania ya leo na Dunia nzima kwa ujumla inahitaji watumishi na watu ambao wanaziona fursa zaidi ndani ya rasilimali chache zilizopo na hii inawezekana pale ambapo watumishi au watu husika huichakata vizuri zaidi rasilimali akili ili thamani yake ya kuchambua takwimu na taarifa iongezeke kuruhusu upeo mpana wa kuzalisha fikra mpya katika kuziona fursa mpya na kupunguza utegemezi toka serikali kuu kwa kupunguza kuishi kwa maelekezo” Amesisitiza Dkt. Gwajima.
No comments:
Post a Comment