ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 3, 2020

Kambi Mpya Yanga Usipime

AVIC TOWN Tanzania - Posts | Facebook
AVIC TOWN BUNGALOWS FOR RENT
Avic town Dar es salaam, Tanzania. Africa - YouTube
AVIC TOWN
KIKOSI cha Yanga kimeanza kuzoea mazingira ya kambi mpya ya kishua iliyopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam katika kijiji cha maraha cha Avic Town, huku nyota wa kikosi hicho wakichekelea wakidai inawapa mzuka wa kufanya mambo makubwa msimu huu katika Ligi Kuu Bara.

Kambi hiyo ambayo itaitafuna Yanga karibu Sh 155 milioni kwa msimu mzima, hapo ni mbali na masuala ya misosi na mengine, lakini wachezaji wao wamefichua siku moja tu ya kuwepo kambini hapo imewapa mzuka na kuamini mazingira yanawapa utulivu wa kufanya makubwa msimu huu.

Mbali na wachezaji hao kufichua siri ya utamu wa kambi hiyo, lakini meneja wa klabu hiyo, Hafidh Saleh ameanika kwamba wapo kambini hapo na mpishi wao maalum na ‘menu’ ya wachezaji inapangwa na daktari na kocha mkuu wa timu hiyo, Zlatko Krmpotic kutoka Serbia.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa muda tofauti jana, wachezaji na meneja huyo wa Yanga, walisema mazingira ya kambi ni rafiki kwao katika maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara inayoanza Jumapili.

“Kambi iko vizuri, ni apartiment fulani hivi, kila kitu kinakwenda sawa na wachezaji wameifurajia kwa kweli,” alisema Hafidh.

Meneja huyo alisema kutokana na kambi hiyo kuwa na kila kitu huko huko, imerahisisha hata ratiba yao ya mazoezi ya kila siku akidai kwa yale ya asubuhi yanaanza saa 3 hadi saa 5 na ya jioni yanaanza saa 10 hadi saa 12.

“Wachezaji wanajifua ipasavyo, ratiba yao ya chakula na mazoezi zinakwenda vizuri na wanapata muda wa kutosha kupumzika,” alisema Hafidh na kuongeza; “Kiukweli, kila kitu kiko vizuri.”

Kwa upande wa wachezaji ambao hata hivyo waliomba kuhifadhiwa majina yao walisema kambi ni tamu kinoma na mazingira yanawapa jeuri ya kuamini huu ni msimu wao katika Ligi Kuu Bara.

“Kila kitu kambini kiko vizuri, tunaishi kwa programu, ambayo kiukweli haijawahi kutokea, tunaipenda na kuifuata,” alisema mmoja wa nyota hao wa Yanga, aliyeungwa mkono na mwingine aliyesema kuanzia programu ya mazoezi, chakula na ratiba ya kupumzika kwenye kambi hiyo si vya kitoto.

“Ni kambi ambayo hakikaiko ‘fresh’ imekamilika, ina hadhi na kila kitu kinakwenda kwa unyoofu,” alisema.

Kuhusu programu ya kambi hiyo, wachezaji hao walisema wanafanya mazoezi kulingana na programu ya siku hiyo.

“Si kila siku tunafanya mazoezi mara mbili, kuna wakati tuna session ya asubuhi na kuna wakati ya jioni.

“Kama tunafanya asubuhi, tunaamka mapema saa 12, tunakunywa chai kisha tunaanza mazoezi, kambi imekamilika, kuanzia ratiba ya msosi, mazoezi na hata kupumzika,” alisema.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alipoulizwa kuhusu kambi hiyo, alisema anayeweza kuizungumzia ni kocha mkuu.

“Kambi inaendelea Kigamboni kama mlivyosikia, ila kocha mkuu au meneja wa timu ndiyo wanaweza kuisemea kwa sasa,” alisema Mwambusi.

GHARAMA ZAKE SASA
Unaambiwa kambi hiyo ya Yanga kwa siku moja tathmini iliyofanywa na gazeti hili imebaini kuwa wadhamini wa timu hiyo kampuni ya GSM itagharamika zaidi ya Sh 155 milioni kwa ajili ya kambi hiyo iliyowekwa katika eneo la kifahari la Avic Town lililopo Somangira, Kigamboni.

Kiasi hicho cha fedha ambacho GSM itatoboka ni gharama ambazo itapaswa kulipa kama pango la kila nyumba ambayo imekodishwa kwa matumizi ya timu hiyo lakini pia fedha nyingine ni za gharama ya usimamizi, umeme na maji.

Kitendo cha Yanga kutumia eneo hilo kwa ajili ya kambi ya msimu mzima kama ilivyothibitishwa na Ofisa Habari wake Hassan Bumbuli, kimefanya ukubwa wa gharama hiyo ya fedha ambayo malipo yake yatasimamiwa na GSM.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Bumbuli alisema kwa kipindi chote ambacho timu hiyo itakuwa hapa jijini Dar es Salaam, kambi yake itawekwa katika eneo hilo la kifahari lenye kiwanja cha soka, mpira wa kikapu na mabwawa ya kisasa ya kuogelea.

“Tutaondoka baada ya michezo yetu miwili ya hapa Dar es Salaam. Kwa huko mikoani siwezi kukuambia ni hoteli gani ambayo tutaenda kufikia kwa kuwa huwa tunasumbuliwa, lakini baada ya kurudi Dar es Salaam, tutakuwa tunaendelea kukaa pale pale,” alisema Bumbuli.

KAMBI ILIVYO
Uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti umebaini kuwa katika eneo hilo, Yanga imechukua nyumba 15 ambazo inazitumia kwa huduma ya malazi kwa wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi na viongozi wachache kwa ajili ya kuisimamia timu.

Gharama ya kila nyumba moja ambayo wamekodi katika eneo hilo ni kiasi cha Dola 500 (Sh 1, 143,000) kwa mwezi hivyo kwa nyumba 15, kila mwezi, gharama ya jumla itakuwa kiasi cha Dola 7,500 (Sh 17,145,000)

Kwa muda wa miezi nane (8) ambao ligi itachezwa msimu mzima, gharama za jumla kwa nyumba hizo 15, itakuwa ni kiasi cha Dola 60,000 ambazo ni sawa na Sh 137,160,000 kwa thamani ya fedha ya Tanzania.

Lakini ukiondoa kiasi hicho cha Dola 60,000 za pango kwa muda wa miezi nane, pia Yanga italazimika kuingia gharama nyingine ambazo ni ile ya usimamizi wa kila nyumba, maji na umeme.

Gharama za usimamizi wa kila nyumba pekee ni kiasi cha Sh 150,000 hivyo kwa kila mwezi, watalazimika kulipa kiasi cha Sh 2,250,000 na kwa muda wa miezi nane, watalipa Sh. 18 milioni.

Jumla ya fedha hizo za pango kwa miezi nane pamoja na zile za gharama ya usimamizi ukijumlisha na za huduma ya maji na umeme, vinafanya kiasi cha fedha ambacho kitalazimika kulipwa katika kipindi cha kambi kwa msimu mzima kuwa zaidi ya Sh 155 milioni.

Gharama hizo zikawa kubwa zaidi ukijumlisha na zile za chakula, vinywaji, usafiri, posho na matibabu kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa chanzo cha uhakika ndani ya Yanga, katika kambi hiyo, nyumba tano ambazo kila moja ina vyumba vitatu vya kisasa, mchezaji mmoja atatumia chumba kimoja peke yake ambacho kitakuwa na huduma zote muhimu ndani kama vile luninga, huduma ya intaneti na maliwato.

Kitendo cha Yanga kuweka kambi huko Kigamboni, ni muendelezo wa utamaduni ambao umeanza kujengeka kwa timu za Tanzania kuzikacha hoteli na badala yake kuweka kambi katika nyumba za kukodi au hosteli za klabu.

Mtibwa Sugar na Azam FC zenyewe zina hosteli ambazo zimejenga na zinazitumia kwa makazi ya wachezaji wakati Simba, Kagera Sugar na KMC zenyewe zimekodisha nyumba ambazo zinatumia kama makazi ya wachezaji wao na maofisa wa benchi la ufundi pindi zinapokuwa na mechi za nyumbani.

No comments: