Na Ashura Kazinja-Morogoro
JESHI la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Madizini, Kata ya Mtibwa wilayani Mvomero, Shabani Hatibu (50), kwa tuhuma za kumbaka binti yake wa kambo anayesoma darasa la tatu.
Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa (SACP), alisema Septemba mosi, majira ya saa tatu asubuhi huko katika Kijiji cha Madizini, Kata ya Mtibwa mkoani hapa, binti huyo mwenye miaka 15, mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Mtibwa, alibakwa na baba yake huyo wa kambo ambaye ni fundi seremala.
Kamanda Mutafungwa alisema awali binti huyo alilalamika kwa mama yake mzazi aitwae Halima Issa (32) mkulima na mkazi wa Madizini, kuwa anasikia maumivu makali anapojisaidia haja ndogo na kudai kuwa amebakwa mara mbili na baba yake wa kambo, na kwamba alimtishia asiseme kwa mtu yeyote na endapo kama atasema atampiga.
Kamanda Mutafungwa alisema binti huyo alidai kuwa kitendo hicho alifanyiwa Agosti 30 wakati mama yake alipokuwa amesafiri kwenda msibani mjini Morogoro.
Alisema Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa hiyo kutoka kwa mama mzazi wa binti huyo, lilianza upelelezi na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo na kwamba hatua za kumfikisha mahakamani zitafuata mara tu upelelezi utakapokamilika.
Katika tukio jingine lililotokea Agosti 31 saa 1 usiku, katika Mtaa wa Nugutu, Kata ya Kilakala, Manispaa ya Morogoro, mtu mmoja Justine Magana (47) mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Nugutu alikutwa akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya katani ambayo aliifunga kwenye kenchi ndani ya chumba wanacholala watoto wake.
Kamanda Mutafungwa alisema marehemu aliacha ujumbe wa maandishi kwa mke wake aitwaye Adelina Helman usemao ‘sitaki ujaze watu wala usiende kituoni, mpigie wifi yako arudi upesi’.
Alisema mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi na daktari katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kwamba umeshakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa mazishi.
No comments:
Post a Comment