Habari kwa niaba ya GPL
Vyama vya Siasa ambavyo vinatarajia kushirikiana wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu bila kufuata Sheria ya Vyama vya Siasa kama ilivyoainishwa kwenye Kifungu Na.11 (a) cha Sheria hiyo vitakuwa vimevunja sheria.Onyo hilo limetolewa jijini Dodoma na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, wakati alipofanya mahojiano kuhusu msimamo wa ofisi yake kwenye suala la ushirikiano wa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Nyahoza amesema kuwa ushirikiano wa vyama hivyo umeratibiwa vizuri kisheria ambapo vyama vinapohitaji kushirikiana vinapaswa kutumia vikao halali vya chama badala ya utashi wa mtu binafsi. Msajili Msaidizi Nyahoza ameongeza kuwa baada ya vikao halali kupitisha azimio la kufanya ushirikiano vyama husika vinapaswa kuwasilisha mkataba wa ushirikiano Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa miezi mitatu kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza.
“Vyama havijakatazwa kushirikiana bali vimewekewa utaratibu ili Tume ya Uchaguzi pamoja na taasisi zote zinazohusika na uchaguzi ziweze kujiandaa vizuri na kuimarisha ulinzi hasa wakati wa kampeni pamoja na kuvisaidia vyama vingine kuelewa wanashindana na vyama vya aina gani” alisema Nyahoza.
Kuhusu ushirikiano wa vyama vya siasa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020 Msajili Msaidizi Nyahoza ameelezea kuwa mpaka sasa ofisi yake haijapokea mkataba wa makubaliano ya ushirikiano kutoka kwa chama chochote cha siasa hivyo kwa mujibu wa sheria vyama ambavyo vina nia ya kushirikiana vimeshachelewa.
Aidha, Msajili Msaidizi Nyahoza amesema hadi sasa vyama vyenye usajili wa kudumu ni 19 na chama kimoja kina usajili wa muda na maombi ya vyama 16 bado yanafanyiwa upembuzi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake