ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 11, 2020

Zanzibar: Maalim Seif Awekewa Pingamizi Mbili


TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeshindwa kumteua Maalim Seif Sharif Hamad kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT-Wazalendo baada ya kuwekewa pingamizi.

Alhamisi tarehe 10 Septemba 2020, ZEC imewateua 16 kati ya 17 waliochukua fomu na kurudisha kugombea urais wa visiwa hivyo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020.

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Thabiti Faina amesema, Maalim Seif ameshindwa kuteuliwa kutokana na vyama viwili vya DP na Demokrasia Makini kumwekea pingamizi.

Amesema, mapingamizi ya vyama hivyo yanafanana ambayo yanahusu ujazwaji wa fomu za Maalim Seif kutokuwa sahihi.

Mkurugenzi huyo amesema, baada ya Maalim Seif kujibu mapingamizi hayo, tume hiyo itaamua kama ni kumteua au la.

Maalim Seif ndiye mgombea pekee anayewamia kugombea nafasi hiyo mara sita kati ya wote 17 waliojitosa kumrithi Rais Ali Mohamed Shein ambaye ananaliza muda wake kwa mujibu wa Katiba

Alianza kugombea mwaka 1995, 2000,2005,2010 na 2015 kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) na sasa anapambana kugombea mara ya sita kupitia ACT-Wazalendo

Jumanne ya tarehe 8 Septemba 2020, Maalim Seif akizungumza katika Kongamano la Vijana la ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar aligusia taarifa za kuwekewa mapingamizi.

Aliwaeleza vijana hao kuna watu wa vyama vingine wamepanga kumwekea mapingamizi ili asiteuliwe kugombea huku akiwakaribisha kufanya hivyo.

“Nasikia kuna watu washapangwa na vyama vingine kuniwekea pingamizi, nawakaribisha, sababu kuniwekea pingamizi yeye anakuja kutoa haja zake na ushahidi wake na mimi naujua vilevile.”

“Sioni kama kuna pingamizi yoyote kama itasimama juu yangu. Mimi nimezaliwa Mtambwe hamjui ninyi? Ndiyo sifa ya kwanza ya mgombea urais awe Mzanzibar wa kuzaliwa sio Mzanzibar mkaribishi,” alisema Maalim Seif.

Wagombea 16 walioteuliwa na ZEC ambao kesho Ijumaa wanaweza kuanza kampeni ni; Hussein Juma Salim (TLP), Issa Mohamed Zonga (SAU), Said Soud Said (AAFP), Said Issa Mohamed (Chadema), Khamis Fakhi Mgau (NRA) na Mfaume Hamis Hasaan (NLD).

Wengine ni; Dk. Hussein Mwinyi (CCM), Hamad Mohamed (UPDP), Shafii Hassan Suleiman (DP), Othuman Rashid Khamis (CCK), Ameir Hassan Ameir (Demokrasia Makini), Ali Omar Juma (Chaumma), Hamad Rashid (ADC), Juma Ali Khatib (Ada Thadea), Mussa Haji Kombo (CUF) na Mohamed Omar Shaame wa UMD

No comments: