Friday, October 16, 2020

JAMII YATAKIWA KUWEKEZA ELIMU KWA MTOTO WA KIKE

Mkuu wa shule ya sekondari Star High school iliyopo Kata ya Mbuguni Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, Sister Monica Massawe akizungumza kwenye mahafali ya 11 ya shule hiyo.
Mhadhiri wa chuo Kikuu cha Sayansi na Teknologia cha Nelson Mandela, Profesa wa hisabati, Verdiana Grace Masanja akizungumza kwenye mahafali ya 11 ya shule ya sekondari Star High school iliyopo Kata ya Mbuguni Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Mhitimu wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Star High school iliyopo Kata ya Mbuguni Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, Evaline Kilonzo akikabidhiwa zawadi ya cheti cha ufaulu somo la sayansi na mgeni rasmi wa mahafali ya 11 ya shule hiyo, Mhadhiri wa chuo Kikuu cha Sayansi na Teknologia cha Nelson Mandela, Profesa wa hisabati, Verdiana Grace Masanja.

Na Mwandishi wetu, Arumeru

Jamii imetakiwa kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike na siyo kutoa kipaumbele kwa wavulana pekee ili kuweka usawa kwa faida ya wakati ujao.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha sayansi na teknologia cha Nelson Mandela, Profesa wa hisabati Verdiana Grace Masanja, ameyasema hayo kwenye mahafali ya 11 ya shule ya sekondari Star High school ya Mbuguni Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.

Prof Masanja amesema wasichana wakipewa kipaumbele kwenye elimu sawa na wavulana, Taifa kwa ujumla litanufaisha, kwani mwanamke ndiyo mtu wa kwanza kuwa karibu na familia.

Amesema hata kwenye shule bora na zenye vipaji inaonyesha msichana hapewi kipaumbele kama wanavyopewa wavulana hivyo jamii inapaswa ibadilike.

“Tuwekeze kwa wasichana kwenye elimu na tuwape nasaha za kujichunga kwani njia ya binti ni ngumu kuliko mvulana kuna vishawishi vingi hadi afauli,’ amesema Prof Masanja.

Mkuu wa Star high school, Sister Monica Massawe amesema shule hiyo ilianzishwa na shirika la kimisionari la Mitume wa Yesu, Januari 20 mwaka 2007.

Sister Massawe amesema shule hiyo ilifanya mahafali ya kwanza ya kidato cha nne mwaka 2010 na hadi sasa wanafunzi 916 wameshahitimu kidato cha nne.

Amesema kwa mwaka huu wanafunzi 84 wamehitimu elimu ya sekondari kidato cha nne wakiwemo wavulana 63 na wasichana 21.

Amesema anawapongeza wahitimu hao kwani wametumia fursa walizozipata za miundombinu bora ya maabara za sayansi, maktaba, walimu na walezi hivyo wajiandae kuendelea na kidato cha sita na vyuo.

Mmoja kati ya wahitimu wa shule hiyo, Evaline Kilonzo amesema amebobea kwenye masomo ya sayansi na lengo lake ni kuwa mwanaanga au daktari.

Mhitimu mwingine Salome Frederick amesema wamejifunza ujasiriamali wa kilimo cha chakula, mboga na matunda na utunzaji mazingira kwa kipanda miti.

Mkurugenzi wa STEMM, John Lidgett amewapongeza walimu na uongozi wa shule hiyo ndiyo sababu shirika hilo lina watoto 10 wanaosoma hapo Star high school

No comments: