Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati.
Na, Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, inamshikilia mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Orkitikiti, Oscar Waluye kwa tuhuma za kufanya udanganyifu katika mitihani ya darasa la saba inayoendelea kufanyika nchini.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu, amesema mwalimu mkuu huyo Waluye wa shule ya msingi Orkitikiti kwenye kijiji Cha Engong’ongare anatuhumiwa kufanya tukio hilo Octoba 7 shuleni hapo.
Makungu amesema mwalimu huyo anatuhumiwa kuwalazimisha wanafunzi wawili wa darasa la sita kufanya mitihani ya darasa la saba.
Amesema lengo la wanafunzi hao kufanya hivyo ni kuwasaidia wengine badala ya watahiniwa ambao uwezo wao darasani umeonekana ni wa kiwango cha chini.
Amesema pia mwalimu mkuu huyo anatuhumiwa kwa kukaririsha mwanafunzi mmoja.
“Wanafunzi hao wawili wa darasa la sita na mwanafunzi mmoja aliyehitimu mwaka jana walikamatwa na makachero wa TAKUKURU tayari wakiwa wameshafanya mitihani ya masomo ya kiswahili na hisabati,” amesema Makungu.
Amesema wanafunzi hao walishafanya mitihani hiyo kwa niaba ya wenzao hao wa darasa la saba wanaodaiwa kuwa na uwezo mdogo huku aliyekaririshwa akitumia jina la mwanafunzi mtoro.
Amesema uchunguzi wa shauri hilo unaendelea na mara utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mwalimu mkuu huyo.
“Ni rai yetu kwa walimu wote nchini kufanya kazi zao kwa uadilifu kwa kuwalea watoto katika njia iwapasayo, ikiwa ni pamoja na kusoma kwa bidii na kujiamini nao hawataiacha hata wakiwa wazee, (Biblia Mithali 22:6),” amesema Makungu.
Amesema badala ya kuwafundisha kuwa tegemezi kwa kufaulisha mitihani bila ya kustahili.
No comments:
Post a Comment