Saturday, December 5, 2020

NAIBU KATIBU MKUU,WIZARA YA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO AWAFUNDA VIJANA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA


Jane Edward fullshangweblog,Arusha

Naibu Katibu mkuu wizara ya Ujenzi uchukuzi na mawasiliano Sekta ya mawasiliano Dkt. Jim Yonazi amesema ni vema wabunifu waliopo katika jamii wakatambuliwa bila kuangalia kuwa ni wanafunzi katika vyuo mbalimbali ili waweze kuendelezwa katika ubunifu wao.

Dkt Yonaz ameyasema hayo wakati akifungua kongamano la ubunifu kwa vijana mkoani Arusha lililofanyika katika Chuo cha Uhasibu Kilichopo Njiro mkoani hapa.

Aidha Dkt. Yonaz alisema wapo wabunifu wengi katika jamii lakini hawatambuliwi kutokana na kwamba siyo wanafunzi wa vyuo hivyo kazi zao hazijatambuliwa.

“Wabunifu ambao hawapo vyuoni watambuliwe ili waweze kuendelezwa msiishie hapa tu chuoni hapana, jamii inawatu wanaobuni vitu mbalimbali lakini hawajaletwa pamoja kama ambavyo mnakusanya vijana kutoka vyuo mbalimbali kuonyesha ubunifu wao” alisema.

Alitoa pia maagizo kwa wanatehama kujisajili katika tume ya Tehama lengo likiwa kupata haki zao za Msingi kupitia Tume ambapo alivitaka vyuo vilivyoanzisha vituo vya kuleta vijana pamoja kuhakiki kila baada ya makongamano wanayoandaa wanapeleka majina katika tume hiyo ili washiriki wa kongamano waweze kutambuliwa.

Naye mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha Prof. Eliamani Sedoyeka alisema kutokana na uhitaji wa vijana kuwa mkubwa wa kutaka kuonyesha bunifu zao waliona waanzishe kituo cha uvumbuzi (Innovation Summit)kwa ajili ya makongamano ya vijana kuonyesha ubunifu mbalimbali.

“Tumefanikiwa kutoa vijana 100 wanaoweza kujitegemea kwa kuweza kusimamia Kazi zao za ujasiriamali bila kusubiri ajira peke yake, na tunashukuru Ofisi ya mkurugenzi Arusha imetupa ushirikiano kwa kiasi kikubwa kwani Mkurugenzi ameahidi kutoa sapoti kwa makundi yaliyokidhi vigezo katika zile asilimia tano za vijana zinazotolewa na jiji” alisema Prof Sedoyeka.

Naye mkurugenzi wa jiji hilo Dkt John Pima alisema watatoa ushirikiano 100% kwa vikundi vitakavyo kidhi vigezo vya kupewa mikopo hiyo kama kutambua mchango wa vijana katika serikali ya awamu ya tano.

Kwa upande wake msimamizi wa Kongamano hilo bi Pamela Choga alisema mashindano ya ubunifu yalifunguliwa rasmi nov 23 mwaka huu na yaliruhusu kila kijana kuonyesha kazi zake za ubunifu ambapo hatua ya kwanza washiriki walitakiwa kuonyesha video fupi inayoonyesha kazi alizobuni, na hatua ya mwisho ni kushiriki kwa njia ya kuonyesha bidhaa mbalimbali zilizobuniwa na baadaye washindi walipatiwa zawadi.

Mshindi wa kwanza hadi wa tatu kila kundi alipatiwa zawadi na cheti cha ushiriki ambapo mshindi wa kwanza alipatiwa fedha taslimu sh. 500,000 , mshindi wa pili sh. Laki tatu na wa tatu sh. Laki mbili.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake