ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 3, 2021

Aida Khenan; Mbunge Pekee Aliyeangusha Mbuyu

MMOJA wa wanasiasa walioibua gumzo mwaka 2020, ni Aida Kheinan. Ndiye mbunge pekee wa kuchaguliwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka jana.

Aida ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini. Ameandika historia ya kipekee kwenye jimbo na Mkoa wa Rukwa kwa jumla.

Mbali na kuwa mbunge pekee wa kuchaguliwa Chadema, ni mbunge wa kwanza mwanamke kwenye Jimbo la Nkasi Kaskazini ambalo awali lilikuwa mikononi mwa kada machachari ‘mbuyu’ wa CCM, Ally Keisy.

Aida ni mbunge wa kwanza wa upinzani katika Mkoa wa Rukwa. Hii yote inaonesha ni namna gani mwanamama huyu alivyokuwa na ngekewa licha ya kuonesha ujasiri na jihada kubwa katika ulingo wa kisiasa.

SAFARI KISIASA

Hata hivyo, Aida ambaye ni miongoni mwa wanawake 26 walioshinda kwenye majimbo 264 ya vyama vyote, alijizolea umaarufu kutokana na hoja zake katika Bunge la 11.

Awali, Aida alikuwa Mbunge wa Viti Maalum; nafasi ambayo aliitumikia kuanzia mwaka 2015 hadi 2020. Ni nafasi ambayo imeonekana kumjenga kisiasa hali ambayo inawapa motisha wadau wa siasa wanaomfahamu na kumwelezea kuwa ni mwanamke jasiri mwenye uwezo wa kutetea hoja na kuijenga pindi anapoiwasili bungeni.

Uhodari wake katika kuuliza maswali na ushiriki wake katika shughuli mbalimbali za jimbo la Nkasi, ni moja ya mambo yanayoelezwa kumbeba katika uchaguzi huo.

Ndiyo maana ilipotimu saa 5:00 usiku wa Oktoba 29, mwaka jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Missana Kwangura kutangaza jina la Aida kuwa mshindi, wengi walipigwa butwaa licha ya anguko kubwa lililoikumba Chadema kwa upande wa majimbo.

SIRI YA USHINDI

Akizungumzia ushindi wake, mbali na kumshukuru Mungu, Aida anasema kiuhalisia Nkasi ilikuwa na ushindani mkubwa kuanzia kipindi cha kampeni hadi uchaguzi.

Pamoja na mambo mengine anasema mila na desturi ndiyo imewafanya wanawake kuwa nyuma katika kusaka nafasi za kisiasa katika mkoa huo.

“Jamii ilikuwa inaamini mwanamke hawezi kufikia malengo aliyokusudia. Lakini bado kulikuwa na dhana ya kwamba, huyu ni mwanamke tu, atafanya nini tukimpa uongozi? Bado ipo, lakini kupitia mimi inaweza kumalizika.

“Ikumbukwe kabla ya kuwa mbunge nimekuwa mwenyekiti wa vijana wa chama mkoa, pia nimewahi kugombea nafasi ya mwenyekiti mkoa wa chama (Chadema). Kwa hiyo uzoefu huo ulinijengea ujasiri wa kuamini hata nafasi nyingine ninaweza,” anasema.

Anasema kilimchosaidia zaidi hata alipokuwa mbunge wa viti maalum Bunge la 11, alipigania mahitaji ya wananchi bila kuangalia itikadi yake.

“Ndiyo maana nimepigiwa kura nyingi na wenye vyama na wasiokuwa na vyama. Sababu nyingine ya ushindi wangu inachagizwa na dosari za mbunge aliyemaliza muda wake pamoja na kushambuliwa kijinsia.

“Kwa jumla, uzoefu, uwezo wa kujiamini, changamoto za jimbo na mabadiliko ya mtazamo kwenye jamii ndiyo sababu za ushindi wangu.

“Wananchi wameniamini kwa hiyo ninatakiwa kubeba imani hiyo ili kuwaonesha mwanamke anaweza kuleta mabadiliko ndani ya jimbo, inawezekana kasumba ya kutomwamini mwanamke ikapotea, lakini nikifanya vibaya, ninaweza kufunga kabisa nafasi ya mwanamke ndani ya jamii yetu,” anasema.

VIZINGITI

Jimbo hilo lenye kata 17 ni moja ya majimbo mawili ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa iliyoanzishwa mwaka 1983, likiwa na rekodi ya kupata uwakilishi wa viongozi wanaume bungeni tangu uchaguzi wa kwanza wa 1995 chini ya mfumo wa vyama vingi kabla ya Aida kuandika rekodi mpya.

Hata hivyo, kizingiti hicho cha ujinsia kinaweza kumpa changamoto Aida iwapo wananchi wa mkoa huo wataendelea kuendekeza mfumo dume na chuki za kisiasa.

Hata hivyo, kwa kuwa wananchi wamemchagua kwa kura 21,226 huku Keissy akiambulia kura 19,972, ni dhahiri kuwa suala la ujinsia wameliweka kando, kinachobaki sasa ni viongozi wa ngazi zote kumpatia ushirikiano katika utendaji wake.

Kizingiti kingine kinachoweza kumpa wakati mgumu Aida ni wingi wa madiwani. Kwa sababu Chadema imepata madiwani wanne pekee kati ya madiwani hao 17.

Hii ina maana kuwa CCM itaunda safu zote za uongozi katika halmashauri na majimbo hayo.

Dk George Kahangwa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema kwa kuwa, Aida anatoka chama cha upinzani hivyo anaweza kukumbana na mikinzano mbalimbali ya hoja zitakazolazimishwa kupitishwa kwa kigezo cha wingi wa kura licha ya kuwa hazitokuwa na tija kwa wananchi.

“Hilo litakuwa lengo mojawapo la kumuangusha au kumjengea taswira hasi ndani ya uongozi wake kwenye jimbo hilo,” anasema.

Hicho ni kizingiti kimojawapo ambacho mwanamama huyo anatakiwa kukivuka kwa kuweka utaratibu dhabiti wa kukutana na wananchi wake kila mara ili apate wasaa mzuri wa kuwaeleza kila jambo linaloendelea kwenye vikao vya baraza la madiwani.

Kwa upande wa bungeni nako, ufinyu wa wabunge wa upinzani ni jambo lingine ambalo linaweza kumfanya ajihisi mpweke.

Dk Kahangwa anasema yamkini wale wabunge 19 wa viti maalumu Chadema wanaweza kurudishwa, hilo litakuwa jambo jema ambalo litamuongezea nguvu Aida, lakini wasiporejeshwa basi itakuwa kazi nyingine kuungana na wabunge wa ACT-Wazalendo na CUF katika kupambana na CCM ndani ya Bunge hilo la 12.

Hata Aida anasema; “Tukiwa ndani ya jengo nitajisikia mpweke kidogo kwa maisha niliyozoea miaka mitano iliyopita, lakini kwa kuwa nilichaguliwa na wananchi wa Nkasi Kaskazini na siyo wengine, kifikra nitakuwa huru kabisa na salama kabisa nikitegemea ujasiri wa wapiga kura wangu. Naamini chama changu kitanipatia baraka zote kuwakilisha wananchi wa jimbo letu,”

CHANGAMOTO

Pamoja na mambo mengine mbunge huyo anasema kipaumbele chake kwa wananchi ni katika mambo manne ambayo ni huduma za maji, afya, elimu na barabara.

Anasema kuhusu upande wa changamoto za mwanamke, anatamani kushughulikia maeneo mengi ambayo Serikali haikufanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“Kwa mfano, jimbo hilo ni kinara wa mimba za utotoni mkoani Rukwa. Pili, wanafunzi wa kike wanasoma umbali mrefu. Takriban asilimia 40 ya vijiji 49 hakuna shule za msingi.

“Tatu, watoto wa kike wanafuata maji umbali mrefu kwa sababu ya changamoto ya maji. Asilimia 32 ya vijiji hivyo hakuna maji licha ya kuzungukwa na ziwa Tanganyika. Tunafikiria kila kitongoji tuwe na kisima kirefu ndani ya miaka mitano ijayo.

“Jambo la nne, ni changamoto ya huduma za afya, wajawazito wanatembea umbali mrefu kwenda kujifungua. Kuna wastani wa asilimia 20 tu ya kata 17 ndiyo kuna vituo vya afya. Sera ya afya inataka kila kijiji kiwe na kituo cha afya, lakini haijatekelezeka bado,” anasema.

Makala; Gabriel Mushi, Bongo, GPL

No comments: