ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, January 6, 2021

GEKUL ‘AWASHUKIA’ MAAFISA UVUVI WANAOSHIRIKIANA NA WAHALIFU

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akikagua moja ya nyavu inayozalishwa katika Kiwanda cha kutengeneza nyavu za kuvulia Samaki, Nyamagara kilichopo Chanika, jijini Dar es Salaam alipokitembelea Januari 5, 2021.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wakwanza kushoto) akiwaeleza jambo Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) alipotembelea maabara wanayoitumia wanafunzi hao kuchunguza magonjwa ya mifugo kilichopo jijini Dar es Salaam Januari 5, 2021. Katikati ni Mtendaji Mkuu, Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene.
Wafanyakazi wa Kiwanda cha kuchakata Samaki, Alpha wakimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa kwanza kulia) Minofu ya Samaki aina ya Pweza ambayo imechakatwa katika Kiwandani hicho kilichopo jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alikitembelea kiwanda hicho Januari 5, 2021.

Na Mbaraka Kambona,

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amesema kuwa hakuna haja ya kuendelea kuwa na Maafisa Uvuvi ambao wanashirikiana na wahalifu kufanya vitendo vya hujuma wakati kuna vijana wengi wenye nia njema ya kulitumikia Taifa wanahangaika na ajira.

Gekul aliyasema hayo alipotembelea Kiwanda cha kuchakata samaki, Alpha kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam Januari 5, 2021.

Kwa mujibu wa Gekul sehemu kubwa ya upungufu wa rasilimali za uvuvi unachangiwa na baadhi ya Maafisa Uvuvi ambao sio waaminifu ambao wamekuwa wakishirikiana na wahalifu kufanya uvuvi usioendelevu unaopelekea kupungua kwa samaki.

“Tulikuwa Kanda ya ziwa, na hapa pia kilio ni hicho hicho malighafi, malighafi zinapungua kwa sababu baadhi ya maafisa uvuvi wanashiriki katika vitendo vya uvuvi haramu, wanashirikiana na wahalifu, hata pale ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vinapotaka kufanya operesheni ya kuwakamata wahalifu wamekuwa wakitoa taarifa kwa wahalifu hao kama ambavyo ilitokea hivi karibuni kule Wilayani Babati,”alisema Gekul

“Kwa nini tuendelee na watu wa namna hii wakati kuna vijana wengi wenye nia njema na taifa lao wapo huko nje hawana ajira na huku ndani ya serikali kuna baadhi ya watu wanahujumu taifa na uchumi wa nchi, hatuna haja kuendelea kuwa na watu kama hawa,” alisisitiza Gekul

Aliendelea kusema kuwa itakuwa aibu wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza hapa nchini halafu washindwe kuendelea na uzalishaji kwa kukosa malighafi kutokana na kushindwa kudhibiti uvuvi haramu.

Aliongeza kuwa wawekezaji ni muhimu kwa uchumi wa taifa kwa sababu wanalipa kodi na tozo mbalimbali ambazo zinasaidia kukuza pato la taifa, uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa vijana.

Aidha, aliwataka maafisa hao ambao wanaojihusisha na vitendo hivyo kujirekebisha na washirikiane kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kwa pamoja waweze kukomesha vitendo hivyo kwa lengo la kunusuru rasilimali za uvuvi.

“Tutimize wajibu wetu tukijuwa kuwa uvuvi haramu ukiendelea tutaviua hivi viwanda na matokeo yake ajira nazo kwa vijana wetu zitapotea,” alieleza Gekul

Gekul aliwataka maafisa uvuvi wote nchini kuendelea kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali iliyopo ya upotevu wa rasilimali za uvuvi katika maeneo yote yalipo maji na maziwa.

Awali, Meneja wa Uzalishaji wa Kiwanda cha Alpha, Sreejish Srinivasan wakati akitoa taarifa ya uzalishaji wa kiwanda hicho alieleza kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uchache wa malighafi kwa ajili ya kuchakatwa kiwandani hapo na mpaka sasa wanafanya shughuli zao chini ya asilimia 15 ya uwezo wa kiwanda hicho.

No comments: