Sunday, January 3, 2021

NAIBU WAZIRI WA MAJI ASIKITISHWA NA UTENDAJI MBOVU WA RUWASA

Naibu Waziri wa Maji Mh Marryprisca Mahundi akizungumza na watendaji wa Wakala wa Maji Vijijini RUWASA wakati alipokagua mradi wa Maji unaotekelezwa wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesikitishwa na utendaji mbovu wa kazi wa watumishi wa Wakala wa Maji Vijijini(RUWASA) Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa kutoa taarifa za uongo na kutelekeza miradi licha ya serikali kutoa fedha.

Akitoa taarifa mbele ya Naibu Waziri katika ziara yake ya kutembelea Wilaya ya Mbarali Meneja wa Wakala wa Maji vijijini(RUWASA)Wilaya hiyo Job Mwakasala alisema upatikanaji wa maji ni asilimia sitini na tisa pointi tisa sita na Rujewa asilimia sitini na saba pointi nne na pia kuna miradi mbalimbali inatekelezwa ikiwemo tisa ya vijijini na mmoja wa mjini.

Mwakasala alisema mradi wa Ruduga Mawindi unatekelezwa kwa awamu tangu 2014/2015 ambao utavifikia vijiji sita utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni kumi na mbili ambapo mpaka sasa umetumia zaidi ya shilingi bilioni nne.

Taarifa hiyo ya upatikanaji wa maji ilipingwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Reuben Mfune ambaye alisema maji yanayopatikana kwa mgao ni chini ya asilimia thelathini pia watendaji wa RUWASA hawana ushirikiano.

Mfune alisema mradi huo umechukua zaidi ya miaka saba na bado unasua sua licha ya fedha kutolewa na serikali.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Mbeya Suma Fyandomo alisema ni wakati sasa wa watendaji wa RUWASA kushirikiana na wananchi ili kumtua ndoo kichwani.

Fyandomo alisema wakati wakiomba kura waliwaaminisha wananchi kuwa CCM itawaletea maji wananchi hivyo ni jukumu la watendaji wa RUWASA kuitekeleza kwa wakati.

Aidha Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Hashimu Mwalyawa alisema Wilaya ya Mbarali inachangamoto katika miradi mingi na hata iliyokwisha haitoi maji.

Meneja Mkuu wa RUWASA nchini Clement Kivegalo alisema atahakikisha miradi inatekelezwa kwa kasi ili ifikapo mwezi machi iwe imefikia hatua nzuri.

“Nimeisikia taarifa ya mhandisi wa Wilaya ni kweli hali ya upatikanaji ni mbaya kutokana na uchakavu wa miundo mbinu mingi”alisema Kivegalo.

Kivegalo alisema fedha inatolewa kutokana na kasi hivyo watendaji wengi hawaendi na kasi katika utekelezaji.

Akitoa hotuba yake Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi alisikitishwa na utendaji mbovu wa Mhandisi Job Mwakasala kwa kushindwa kutoa taarifa sahihi ya miradi na kutelekeza mabomba ya mradi wa Ruduga Mawindi tangu mwezi august mwaka jana.

Mahundi ameagiza meneja huyo aondolewe na kupangiwa majukumu mengine.
Baada ya kutoridhishwa na maendeleo ya mradi huo katika kijiji cha Kangaga kitongoji cha Mkondo Kata ya Mawindi Mahundi alitembelea mradi wa Uhamila ambapo Diwani wa Kata ya Rujewa Michael Jeremiah Makao alisema pamoja na kukamilika kwa mradi huo zaidi ya miaka kumi wananchi hawapati maji.

Alipopigiwa simu Meneja wa RUWASA Rujewa alisema mradi wa Uhamila unatoa maji kauli iliyomchefua Naibu Waziri na kuagiza aondolewe kwenye nafasi hiyo mara moja.

Kama haitoshi Naibu Waziri alitembelea mradi wa Imalilosongwe ambao nao hautoi maji kwa kile kilichodaiwa kuwa tanki ni dogo halisambazi maji ipasavyo.

Diwani wa Kata ya Imalilosongwe Chuki Jeremiah alisema wataalam wanakwamisha juhudi za serikali hivyo kuleta kero kwa wananchi.

Naibu Waziri alihitimisha ziara yake Mkoani Mbeya kwa kutembelea mradi wa kisima Ilongo ulioanza mwaka 2018 lakini haujakamilika licha ya kuwepo shilingi milioni sabini benki.

No comments: