Thursday, January 7, 2021

SAFARI YA MWISHO YA MTOTO WA MWALIM NYERERE,WAZIRI MKUU AONGOZA MAZISHI

Waziri Mkuu Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kassim Majaliwa jana ameshiriki mazishi ya mtoto wa Marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rosemary Nyerere aliyefariki dunia Januari Mosi, 2021.

Mazishi hayo ya Rosemary Nyerere yamefanyika hapo jana Januari 6, 2021 katika makaburi ya Kanisa Katoliki yaliyopo kwenye Kituo cha Hija kilichoko Pugu jijini Dar es Salaam.

Ibada ya mazishi imeongozwa na Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki Upanga jijini Dar es Salaam, Dias Mario. Viongozi wengine walioshiriki katika mazishi hayo ni pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Mkewe Mama Sitti, Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba.

Wengine ni mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa, Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenyeulemavu, Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula.

Viongozi wengine ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi, Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakary Kunenge na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake