KATIKA kuitikia mwito wa kujenga mshikamano na kuimarisha afya mahali pa kazi, Watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina leo walijitokeza kwa wingi kushiriki katika bonanza la michezo lililoandaliwa na ofisi hiyo.
Mbali ya kujitokeza kwa wingi, wengi wao walionekana kung'ara katika michezo waliyoshiriki ikiwemo ya soka, kuvuta kamba, riadha, kukimbiza kuku na mbio za magunia.
Akizungumza katika viwanja vya michezo vya Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Pili Mazowea amemshukuru Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka kwa kuwawezesha kufanikisha bonanza hilo na kusema kuwa lengo la michezo hiyo ni kujenga umoja, upendo na ushirikiano wa pamoja baina ya watumishi wake.
Aidha, ameongeza kuwa, michezo hiyo itawasaidia watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuimarisha afya zao na kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi na ufanisi wakiwa wenye afya njema.
"Tutaimarisha afya zetu ambazo zitatufanya tuweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi," alisema Mazowea.
Mkurugenzi huyo amewashukuru washiriki katika bonanza hilo na kuwaomba wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki wajitahidi kwa mara nyingine waweze kufanya hivyo ili kuimarisha umoja katika ofisi hiyo yenye jukumu la kusimamia taasisi, mashirika ya umma na wakala wa Serikali, ili kuleta tija kwa Serikali kupitia uwekezaji wake.
No comments:
Post a Comment