Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hassan Abbasi; Kaimu Katibu Mtendaji wa BMT, Bibi Neema Msita, Rais wa TFF, Bw. Wallace Karia na Katibu wake Mkuu, Bw. Wilfred Kidau; Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Bw. Stephen Mghuto na Mtendaji wake Mkuu, Bw. Almas Kasongo; Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Bw. Murtaza Mangungu na Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba Barbara Gonzalez na Mjumbe wa Bodi ya Simba, Zacharia Hanspoppe; na kwa upande wa Yanga alihudhuria Mwenyekiti wa Yanga Dkt. Mshindo Msolla aliyeambatana na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Yanga, Mhandisi Bahati Mwaseba na Kaimu Katibu Mkuu CPA Haji Mfikirwa.
Baada ya majadiliano ya kina kuhusu sababu, mazingira ya kabla, wakati mchezo huo uliposogezwa mbele kwa saa chache na baada ya mchezo huo kulazimika kuahirishwa, makubaliano yenye nia njema kuhusu hatma mbalimbali za mchezo huo yamefikiwa na Wizara kwa niaba ya Serikali hivyo Serikali inatoa maelezo na maelekezo yafuatayo:
1. Kuhusu hatima ya Mechi ya Simba na Yanga iliyoahirishwa: Makubaliano yamefikiwa kuwa mechi hiyo irudiwe ili kuwapa wapenzi wa soka kile walichokitarajia na Wizara inaliacha suala hili katika taratibu za TFF na Bodi ya Ligi ambayo ina uwakilishi wa Vilabu mbalimbali ili wakae haraka iwezekanavyo na kutoa tarehe ya kurudiwa mechi hiyo;
2. Kuhusu hatma ya mashabiki waliokata tiketi na kutoona mechi kusudiwa: Makubaliano yamefikiwa na Mhe Waziri ametoa maagizo kwa Kituo cha Kitaifa cha Data (Data Center) wanaosimamia mfumo wa N-Card unaotumika kununua tiketi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuwarejeshea tiketi zao kwenye mfumo wa kadi za kuingilia uwanjani mashabiki wote 43, 947, ili tiketi hizo hizo za kielektroniki ziwasaidie kuingia tena uwanjani kwa kila mmoja kukaa eneo lile lile alilokata awali siku na tarehe itakayopangwa kurudiwa mechi ya Simba na Yanga;
3. Kuhusu haki za mashabiki wengine wapya watakaopenda kuingia uwanjani: Mhe Waziri ameagiza, pamoja na mashabiki hao 43,948 kurejeshewa tiketi zao, mfumo wa N-Card pia uruhusu kuuzwa tiketi zaidi kupitia N-Card kwa mashabiki wapya watakaoamua kuingia uwanjani siku hiyo hadi kufikia au kukidhi idadi inayoruhusiwa kulingana na uwezo wa uwanja; na
4. Juu ya hali ya sintofahamu na kutokuaminiana kati ya baadhi ya Vilabu na TFF: Kwa kuwa imeonekana kuna hali ya sintofahamu kubwa kati ya baadhi ya vilabu hususani Yanga na TFF, na kwamba licha ya vikao vya awali kati ya TFF, Yanga na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Michezo, Bw. Yusuph Singo, bado hali hiyo inazidi kumea hivyo,Mhe Waziri ameahidi kuitisha kikao kingine haraka kati ya pande hizo mbili ili kujadili changamoto na kuondoa jakamoyo iliyopo. Tarehe za kikao hicho zitapangwa katika siku za hivi karibuni.
Mwisho, Mhe. Waziri, kupitia kwa watendaji wa vilabu hivyo, naye amerejea kuwaomba radhi mashabiki na wapenzi wa soka nchini kufuatia kusogezwa mbele kwa saa kadhaa na baadaye kuahirishwa kwa mechi ya Simba na Yanga iliyokuwa ichezwe Mei 8 mwaka huu.
Hata hivyo, amewaomba viongozi wa vilabu na mashabiki kuwa watulivu katika kipindi hiki na kuiamini Serikali kuwa ilikuwa na nia njema na sababu za msingi iliposhauri awali kwa wadau wa mchezo huo kuwa mechi isogezwe mbele kwa saa chache kabla ya kujitokeza mazingira yaliyosababisha Bodi ya Ligi kulazimika kuahirisha kabisa mchezo huo.
No comments:
Post a Comment