ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 9, 2021

MAWAZIRI WA FEDHA NA UCHUMI WA EAC WAKUBALIANA KUBORESHA TUME YA KISWAHILI

Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Fedha na Uchumi (SCFEA) pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Mashauriano ya Kibajeti umefanyika jijini Arusha leo tarehe 7 Mei 2021 huku Mawaziri hao wakikubaliana na hoja ya kuiboresha Tume ya Kiswahili ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi badala ya kuivunja.

Awali hoja ya kuivunja Tume ya Kiswahili iliwasilishwa kupitia ripoti ya mshauri mwelekezi na kuungwa mkono na takriban Nchi zote Wanachama isipokuwa Tanzania kama moja ya mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji ndani ya Jumuiya. Hata hivyo,nchi hizo ziliafiki kwa kauli moja hoja zilizolizotolewa na Tanzania kuhusu umuhimu wa Tume hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba alieleza umuhimu wa Tume hiyo na kwamba ni kielelezo pekee muhimu cha Jumuiya na kuwataka kuunga mkono hoja ya kuiboresha na kuiimarisha ili iendelee kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

“Hoja ya kuvunja Tume ya Kiswahili kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji wa Jumuiya inalenga kudidimiza malengo na misingi iliyopo ya kuiunganisha jumuiya. Hivyo nasisitiza kuwa bado upo umuhimu mkubwa wa kuienzi Tume hiyo ambayo ni kielelezo muhimu cha Jumuiya badala ya kufikiria kuivunja” alisema Mhe. Nchemba.

Awali, akifungua mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Waziri wa Fedha wa Kenya, Mhe. Ukur Yatani Kanacho, alisema ana matarajio makubwa mkutano huo utafanyika kwa mafanikio na kutoa pole kwa niaba ya Mawaziri walioshiriki Mkutano huo kwa Ujumbe wa Tanzania na Serikali kwa ujumla kwa kuondokewa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Pia alitoa pole kwa Nchi Wanachama kufuatia janga la ugonjwa wa Corona na kuwataka wajumbe kuendelea kushirikiana kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbambali zilizowasilishwa ikiwemo taarifa za Kamati zinazoshughulikia masuala ya Fedha ikiwemo ile ya Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Nchi Wanachama pamoja na taarifa ya Utafiti wa kuboresha Mifumo na Miundo ya Uendeshaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kulingana na rasilimali zilizopo.

Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo umewahusisha pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji Uchumi na Ajira Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga, Waziri, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Zanzibar, Bw. Mussa Haji Ali, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina HK. Shaaban na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.

Mkutano huo ambao umeitishwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulitanguliwa na kikao cha Ngazi ya Wataalam kutoka Sekta za Fedha na Uchumi uliofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5 Mei 2021 na kufuatiwa na kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 6 Mei 2021.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza wakati wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha tarehe 7 Mei 2021. Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Wataalam na Makatibu Wakuu vilivyofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 6 Mei 2021. Kulia ni Waziri, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali na kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga akichangia jambo wakati wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Fedha na Uchumi la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kushoto ni Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina HK. Shaaban
Ujumbe wa Burundi ukiongozwa na Mhe. Balozi Ezechiel Nibigira (katikati) wakishiriki Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Wajumbe wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa kwenye Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mhe. Waziri Nchemba kwa pamoja na Mawaziri kutoka Zanzibar wakifuatilia Mkutano. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Uchumi na Ajira Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga
Mhe. Balozi Nibigira kutoka Burundi akichangia jambo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Zanzibar, Bw. Mussa Haji Ali na Kamishna Msaidizi, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. James Msina
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Elias Bagumhe akiwa kwenye Mkutano wa 12 wa Baraza la Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ujumbe wa Tanzania
Sehemu ya ujumbe wa Tanzania
Mkutano ukiendelea
Wajumbe wakifuatilia mkutano
Mkutano ukiendelea

No comments: