ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 12, 2021

Milango ikowazi wadau wa madini kutoa maoni- Biteko

 

Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema mlango wa wizara uko wazi  kwa wadau wa madini nchini kuwasilisha maoni yao juu ya namna bora ya kuboresha na kuendesha Sekta ya Madini ili iweze kuongeza tija kwa nchi na wananchi.
 
Amesema, Sheria zote zinazotukwaza tutarekebisha lakini sheria zinazosimamia maslahi ya nchi na wananchi tutazisimamia.
“Tunatunga sheria kwa ajili yetu, tutafanya marekebisho kwa kuangalia maslahi makubwa ya nchi. Hivyo tutajadili na kufanya marekebisho pale itakapofaa”.

Waziri Biteko ameyasema hayo leo tarehe 12 Mei, 2021 alipokuwa akifungua kikao cha majadiliano baina ya Serikali na Chemba ya Migodi Tanzania (Tanzania Chamber of Mines) kilichofanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.
 
Aidha, Biteko amewataka wadau hao wa madini kuuimba wimbo wa local content ( Ushiriki wa Nchi na Wananchi kwenye Uchumi wa Madini) na kubainisha kuwa endapo tukafanya kosa la kutokuwashirikisha watanzania kwenye uchumi wa madini katu kama taifa na wananchi hawataweza kunufaika na rasilimali madini zilizopo nchini.   

Amesema bidhaa na huduma zinazoweza kutolewa na watanzania zitolewe na  watanzania huku akitoa mfano kuwa endapo tukiruhusu biashara ya Milioni 600 inayoweza kufanyika nchini ifanyike nje ya nchi  wafayabiashara waliopo nchini hawatanufaika bali nchi ambako hizo pesa zimekwenda ndio watakaonufaika.

Akijibu hoja ya kuongeza shughuli za utafiti wa madini nchini, Biteko ametoa wito kwa mwekezaji yeyote anayehitaji kufanya utafiti wa madini nchini asisite kuomba leseni huku akibainisha kuwa  leseni nyingi za utafiti zimetolewa kwa wawekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa, tafiti nyingi za madini zimekwisha fanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) na kuwataka wanaotaka taarifa hizo kutembelea taasisi hiyo ili kupata taarifa Zaidi.

Akizungumzia suala la mitaji, Waziri Biteko amesema kwa sasa mabenki  ya ndani yameitikia wito wa kuwakopesha wachimbaji wakubwa kwa wadogo na wako tayari kuanza kutoa mikopo hiyo ambapo tayari mgodi wa Uchimbaji Mkubwa wa Madini wa Geita (GGM) umenufaika.

Ameongeza kuwa,  Wizara ya Madini na Taasisi zake wataendelea kutoa elimu ya uwekezaji kwenye sekta ya madini kwa taasisi za kifedha yakiwepo mabenki ili kuwa na uelewa Zaidi wa namna biashara ya madini inavyofanyika huku akiitaka Chemba ya Migodi nchini kuhusika katika utoaji wa elimu hiyo kwa mabenki na taasisi nyingine za kifedha ili kuwajengea uwezo katika kufanya kazi na wawekezaji wa sekta ya madini.

Pamoja na mambo mengi aliyozungumzia akifungua majadiliano hayo, Waziri Biteko amewataka wawekezaji hao kuhakikisha wanakuwa na mahusiano na kukubalika katika jamii wanakokwenda kuwekeza ili kuweka urahisi katika kutekeleza majukumu yao huku akiwataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya uwekezaji kwenye masuala ya uchimbaji wa madini kuondoa dhana kuwa wawekezaji katika sekta hiyo wanawanyonya badala yake kila mmoja baina ya mwekezaji na wananchi hutegemeana.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Tanzania Mhandisi Philibert Rweyemamu amesema, kutokana na mchango mkubwa wa Sekta ya Madini kwenye pato la taifa wameona vema kuwa na kikao na Serikali kupitia wizara ya Madini ili kutoa maoni na ushauri wao juu ya sheria zenye ukakasi katika kusimamia sekta ya madini ili iweze kuziboresha na hatimaye kuongeza mchango wake kwa Serikali.

Amesema uhai wa madini ni sawa  na uhai wa migodi, mwisho wa siku itaisha hivyo ni vyema kuwa na sheria zitakazoifanya sekta ya madini kuwa endelevu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa majadiliano hayo, Mjumbe wa Chemba ya Madini Simon Shayo, amesema biashara ya uchimbaji wa madini ni biashara shindani kwani kuna nchi nyingine ambazo migodi inafunguliwa hivyo serikali inapaswa kuweka mazingira rafiki ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia usalama wa uwekezaji wao ili wawekezaji  waone sababu ya kuja kuwekeza nchini.

Aidha, amekiri kuona  mwamko mkubwa wa serikali katika kuwasikiliza wawekezaji na zaidi katima kutatua changamoto zao. 

No comments: