ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 13, 2021

Taarifa Ya Chama Cha Mapinduzi Kuhusu Mwenendo Wa Kampeni Za CCM Majimbo Ya Buhigwe Na Muhambwe Kuelekea Uchaguzi Wa Marudio

 


Chama Cha Mapinduzi kilifanya uzinduzi wa kampeni za ubunge katika Jimbo la Muhambwe tarehe 4 Mei 2021 na Jimbo la Buhigwe tarehe 5 Mei 2021 ukiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Ndugu Kassim Majaliwa.

Chaguzi hizi ni kutokana na kufariki kwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe Ndg. Atashasta Nditye na Mbunge wa Buhigwe, Ndugu Philip Mpango aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ifuatayo ni tathimini fupi ya Kampeni za Uchaguzi Mdogo wa marudio katika majimbo hayo ya Muhambwe na Buhigwe.

Lengo kubwa la kampeni za CCM ni kutekeleza majukumu yafuatayo;

i.    Kutangaza Sera na Ilani ya CCM, kuwaeleza wananchi jinsi tulivyojipanga kuwaletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

ii.    Kuwanadi kwa wananchi (wapigakura) wagombea wetu Dkt Frolence George Samizi wa Jimbo la Muhambwe na Mwalimu Eliadory Felix Kavejuru wa jimbo la Buhigwe.

Majimbo ya Buhigwe na Muhambwe ni ya CCM. Tulipoteza Mbunge wa CCM kwa kifo kule Muhambwe, hivyo wananchi wanachokitaka ni kuifariji CCM. Kwa Jimbo la Buhigwe wananchi wenyewe wanataka kumpa ahsante Mhe Rais Samia kwa kumteua Makamu wa Rais aliyekuwa mbunge wao Dkt Philip Mpango.

CCM imedhihirisha kivitendo uwezo wake mkubwa wa kuwatumikia wananchi katika awamu zote za uongozi. Kazi kubwa ya kisera na utekelezaji wa miradi, kuondoa kero imefanyika  chini ya CCM kwenye majimbo ya Muhambwe na Buhigwe hivyo ushindi wa CCM ni jambo lisilo na shaka  wala wasiwasi.

Mfumo wa Kampeni kwa Wagombea wetu ulijielekeza katika kufanya zaidi mikutano midogo, kukutana na kuzungumza na makundi ya kijamii katika maeneo yao/makazi/vijiji vyao.

Dkt Florence George Samizi amefika katika Kata zote 19 na amefanya mikutano midogo ya Kampeni na kukutana na makundi maalum ya Vijana, Wanawake, Wazee, Wafanyabiashara na makundi mengine ya kijamii. Wakati wote wa kampeni wananchi wamejitokeza kwa wingi kuhudhuria katika mikutano yetu ya Kampeni jimboni humo na kuonyesha matarajio yao kwa mgombea wa CCM Dkt Samizi.

Ndg  Eliadory Felix Kavejuru amefanya kampeni katika Kata zote 20, na kukutana na wananchi katika Vijiji 44 sawa na asilimia 100 ya vijiji vyote na anaendelea kumalizia kampeni katika vitongoji vinane (8) vilivyobaki kati ya 192.

Mikutano mikubwa imefanywa kimkakati katika viwanja vya Shule ya Msingi Buhigwe, Munanila, na Muyama maeneo hayo yana wakazi wengi  waliojiandikisha katika kupiga  kura. Mikutano midogo 62 aliyoifanya Mgombea wa CCM Ndugu Kavejuru pamoja na mazungumzo mahsusi na makundi ya kijamii yamemkutanisha na kumpa uhakika zaidi wa kupata ushindi .

Chama kimezishirikisha Jumuiya  zake zote katika kampeni za majimbo ya Muhambwe na Buhigwe pamoja na kuwatumia makada wake mbali mbali ambao wote tulia na lengo moja la kupata ushindi.

Viongozo na Makada hao wamekuwa wakihutubia mikutano  ya hadhara kwa kutumia sera za chama Sera nzuri za CCM ambazo zimekuwa zikitekelezeka na kuleta manufaa kwa wananchi

Kampeni za CCM katika Majimbo yote mawili zitafungwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Nd. Philip Isdor Mpango tarehe 14 na 15 Mei 2021 katika uwanja wa Taifa kwa jimbo la Muhambwe na uwanja wa shule ya Mayama kwa jimbo la Buhigwe.

Tathmini ya awali imeonesha katika majimbo hayo CCM itashinda si chini ya 80% na ikumbukwe ushindi huu hautakuwa mgeni kwetu kwani CCM ni kinara na baba wa mageuzi ya demokrasia ya nchini, Afrika Mashariki na Kati.

Nilisema Siku ya uzinduzi na ninaendelea kusisitiza CCM itashinda Buhingwe na Muhambwe  kwa haki, amani na utulivu mkubwa pamoja na yote lakini ya sababu kubwa za ushindi ni imani kubwa walionayo wananchi kwa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi.

Chini ya Uenyekiti wa CCM wa ndugu Samia Suluhu Hassan tutaendelea kuvilea vyama vya siasa chini ili viendelee kufanya siasa safi na yenye tija kwa Taifa baada ya kufanya siasa za danadana. Sote tunajenga nyumba moja hakuna sababu kugombeana fito.

Ikumbukwe kuwa tokea siasa za nchi hii kuanzia TANU hatimae CCM Chama chetu hakijawahi kufanya makosa katika mambo ya msingi yanayohusu maslahi ya Taifa tunakumbusha kuwa uchaguzi wa Buhingwe na Muhambwe umebeba maslahi mapana ya Taifa kwa maana unakwenda kuzalisha wabunge wanakwenda kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hivyo hatuwezi kufanya makosa.

Tumejipanga kuhakikisha Wanachama wetu waliojiandikisha wanajitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura na kuwachagua Wabunge wanaotokana na Chama chao pendwa.

Aidha tunatoa wito kwa vyama vingine na wananchi kwa ujumla kuendelea kudumisha  amani, usalama na utulivu ambao umekuwepo  wakati wote wa kampeni zetu.

Imetolewa na;

SHAKA HAMDU SHAKA
KATIBU WA H/KUU - ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI
13 MEI 2021

No comments: