ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 12, 2021

Wadau Wa Maendeleo Waahidi Kuongeza Kasi Ya Kuisaidia Tanzania Kimaendeleo

 


Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
SERIKALI na Washirika wa Maendeleo wamemaliza mkutano wao wa siku mbili na kukubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano ili kuharakisha maendeleo ya Tanzania kwa kuboresha masuala ya kodi na kuhamasisha ushiriki wa Sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi

Katibu MKuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba ameeleza kuwa mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa ambapo ushauri uliotolewa na washirika wa maendeleo ikiwemo umuhimu wa kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ambao amesema umefanyiwakazi.

“Tumeanza utekelezaji wa mpango wa uboreshaji mazingira ya biashara nchini (blue print) na tunatoa wito kwa Watanzania na wafanyabiashara wengine kutoka ndani na nje ya nchi kufanyabiashara zao kwa uhuru na uwazi hususan kwenye masuala ya kodi ili nchi iweze kupiga hatua kimaendeleo” alisisitiza Bw. Tutuba.

Amewashauri wafanyabiashara nchini pamoja na wawekezaji kutoka nje kutumia fursa za uwekezaji zilizopo nchini kwa kuwekeza mitaji yao hatua itakayokuza biashara na kuongeza ajira.

Bw. Tutuba alisema kuwa Serikali inaendelea na ulipaji wa madeni ya marejesho ya kodi kwa wafanyabiashara na kwamba itaongeza kasi zaidi ya kulipa madeni hayo baada ya kukamilika kwa uhakiki wa madai yaliyoko mezani.

“Tumetengeneza mfumo pale Mamlaka ya Mapato Tanzania utakaotumika kuchakata madai yote ya marejesho ya kodi utakao tusaidia kufanya marejesho haraka na kwa sasa baadhi ya madai yaliyopo yakiwemo ya uagizaji wa sukari tumeanza kuyalipa na tutaendelea kufanya hivyo kadri uhakiki unavyo kamilika” alisema Bw. Tutuba

Bw. Tutuba alirejea wito wake kwa watanzania kudai risiti wanapofanya ununuzi wa bidhaa na huduma pamoja na kuwasisitiza wafanyabiashara kutoa risiti wanapouza bidhaa na huduma kwa kuzingatia thamani ya fedha halisi iliyotolewa ili nchi iwe na uwezo wa kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo ambaye pia ni Kaimu Balozi wa Serikali ya Uswis hapa nchini Mhe. Leo Nascher, aliahidi kuwa washirika wa maendeleo wameridhishwa na uwazi uliopo katika Serikali na kuahidi kuwa watafanya kila linalowezekana kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi yake ya maendeleo kwa manufaa ya taifa na wananchi wake.

Alisema kuwa Mkutano huo umefungua njia zaidi ya ushirikiano na kwamba watahakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inapiga hatua kubwa kimaendeleo na kwamba wao kama washirika wa maendeleo watatoa mchango huo kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaotekelezwa hivi sasa na Mpango mpya wa Awamu ya Tatu utakaoanza kutekelezwa hivi karibuni.

Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha wataalamu kutoka Serikalini na Washirika wa Maendeleo kutoka ofisi za balozi mbalimbali nchini na Mkutano mwingine utakao wakutanisha viongozi mbalimbali ikijumuisha Mawaziri wa sekta mbalimbali, mabalozi kutoka nchi washirika wa maendeleo, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.

No comments: