ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 10, 2021

WAZIRI NDUMBARO ATOA MAAGIZO KWA TANAPA BAADA YA WAZEE KUSALIMISHA SILAHA NA KUTANGAZA KUACHA UJANGILI HADHARANI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akivishwa vazi aina ya Kikoi na Mwakilishi wa Wazee wa Wanawake wa Kijiji cha Kihumbi, Suzana Magori ikiwa ni shukrani mara baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa kuchangia milioni 100 kwa ajili ya kuchangia Ujenzi wa Zahanati katika Kijiji cha Kihumbi kilichopo wilayani Bunda ambayo tangu kukamilika kwake Wanawake wajawaziti wapatao 19 wamejifungua salama.
Mwakilishi wa Wazee wa Kijiji cha Kihumbi, Joseph Mrisho akikabidhi kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro baadhi ya silaha za mfano walizokuwa wakitumia katika Uwindaji haramu wa wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara ambapo Wazee hao wametangaza hadharani kuachana na shughuli hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akiwa ameshika baadhi ya silaha za mfano mara baada ya kuzisalimisha walizokuwa wakitumia katika Uwindaji haramu na katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara. Kulia ni Mbunge wa Bunda Vijijini, Mhe. Boniface Getere.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akiwa kwenye picha ya pamoja na Wazee waliosalimisha baadhi ya silaha za mfano walizokuwa wakitumia katika Uwindaji haramu wa Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara ambapo Wazee hao wametangaza hadharani kuachana na shughuli hiyo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuhakikisha linawasaidia Wazee kufanya shughuli nyingine za kiuchumi kufutia kutangaza hadharani kuacha ujangili na kusalimisha baadhi ya mfano wa silaha za jadi walizokuwa wakizitumia kuua Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Hatua hiyo ya kukabidhi silaha hizo imekuja kufutia TANAPA kuchangia kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga Zahanati ambayo imekamilika na imeanza kuwahudumia Wananchi wa Kijiji hicho ambapo hadi sasa jumla ya Wanawake wajawazito 19 wamejifungua salama.

Ametoa agizo hilo leo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kihumbu kilichopo katika wilaya ya Bunda mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara

Dkt. Ndumbaro amesema kitendo kilichofanywa na Wazee hao kutangaza hadhrani kuachana na uwindani haramu ni jambo la kupongezwa na kila Mtanzania mwenye kupenda shughuli za Uhifadhi nchini.

Kufuati hali hiyo Waziri Dkt. Ndumbaro ametaka Wazee hao kutafutiwa Shughuli nyingine za kiuchumi ambazo ni rafiki kwa uhifadhi ikiwamo ufugaji nyuki.

”Wazee hawa wapeni Mizinga ya nyuki kwa idadi watakayohitaji waweze kufuga nyuki” amesisitiza Dkt. Ndumbaro.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amewashukuru Wazee hao kwa kuonesha mfano bora kwa vijana kuwa Wanyamapori waliopo katika Hifadhi ya Serengeti ni kwa ajili yao na Watanzania wote.

”Wazee wangu nawashukuru sana leo ni siku ya kihistoria katika Kijiji hiki, KItendo cha kukabidhi silaha hizi ni jambo la kuigwa na jamii yote na mumeonesha uelewa mkubwa katika masuala ya Uhifadhi nchini” alisema Dkt. Ndumbaro

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wazee aliyekabidhi silaha hizo, Joseph Mrisho amesema wao kama Wazee wamesukumwa kukusanya na kusalimisha silaha hizo kutokana na TANAPA inavyowachangia katika shughuli zao za Kimaendeleo

Amesema Zahanati hiyo iliyojengwa kwa msaada mkubwa wa fedha kutoka TANAPA umewaadhihirishia Wazee kuwa Wanyamapori ni fedha hivyo hawatakiwi kuwindwa kwa ajili ya Kitoweo.

Kwa Upande wake Mwakilishi wa Wazee kwa upande wa Wanawake, Suzan Magori amesema tangu Zahanati hiyo kukamilika jumla ya akina Mama Wajawazito wameweza kujifungua salama katika Zahanati hiyo ilhali hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma hiyo

” Sisi wanawake tunaishukuru sana TANAPA kwa kutupunguzia adha tuliyokuwa tukiipata hapo awali tunaamini ahata vifo vya akina Wanawake watakaokuwa wakijifungua katika Kijiji hiki kupitia Zahanati hii vitapungua

No comments: