ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 6, 2021

Benki Ya Dunia Yaipatia Tanzania Mkopo Wa Trilioni 2.3


 Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WFM, Dodoma
Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia imeidhinisha mikopo minne yenye masharti nafuu yenye jumla ya dola za Marekani bilioni 1.017 (sawa na shilingi trilioni 2.3391) kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma.

Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa miradi iliyopata idhini ya Bodi hiyo ni mradi wa kuboresha barabara za vijijini (RISE) wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 300 na mradi wa kuimarisha mazingira ya ufundishaji na mafunzo katika taasisi za elimu ya juu (HEET) wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 425.

“Miradi mingine ni mradi wa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao (DTP) wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 150 na Mradi wa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma bora za umeme visiwani Zanzibar wenye mkopo wa dola za Marekani milioni 142,” alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Alieleza kuwa mradi wa kuboresha barabara za vijijini utahusisha ujenzi wa jumla ya kilomita 535 kwa kiwango cha lami katika wilaya sita za mikoa ya Iringa, Lindi, Geita na Tanga na ukarabati wa maeneo korofi ya barabara za vijijini nchi nzima.

Alisema kuwa mradi wa kuimarisha elimu ya juu utaimarisha mazingira ya ufundishaji katika Taasisi za Elimu ya Juu katika fani za kipaumbele cha Taifa, kupitia upya na kuboresha mitaala ya vyuo vikuu ili kuwa na wahitimu wanaoendana na soko la ajira na kuchangia maendeleo ya nchi na uchumi kwa ujumla.

“Mradi wa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao utasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao wa intaneti na kuboresha huduma za umma kwa kutumia digitali kwa kustawisha ekolojia ya digitali nchini, kuhakikisha uunganishaji wa kidigitali kwa Watanzania wote na kuboresha jukwaa la huduma za kidigitali,” alifafanua Mhe. Dkt Nchemba.

Alisema kuwa Mradi wa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma bora za umeme visiwani Zanzibar utasaidia upatikanaji wa huduma bora na za uhakika za umeme visiwani humo ikiwa ni pamoja na kujenga mitambo yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kiwango cha MW 18 kupitia nishati jadidifu ya nguvu ya jua na msongo wa kV132 wa kusafirishia umeme katika visiwa hivyo.

Waziri Dkt. Nchemba aliishukuru Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia, Menejimenti ya Benki ya Dunia Ofisi ya Tanzania, pamoja na Watumishi wote wa Serikali walioshiriki katika kufanikisha upatikanaji wa fedha hizo.

Akizungumzia kuhusu Deni la Taifa alisema kuwa mpaka sasa deni la Serikali ni dola za Marekani milioni 26,416.8 (sawa na Tshs 60.719.01 bilioni) ikijumuisha deni la nje dola za Marekani milioni 18,907.7 na deni la ndani ni dola za Marekani milioni 7,509.1 (sawa na sh. bilioni 17,259.9 na kwamba deni hilo ni himilivu.

Kwa upande wa makusanyo ya mapato ya Serikali Mhe. Dkt. Nchemba alisema yanaendelea vizuri ambapo lengo la makusanyo kwa kipindi cha miezi mitatu toka Februari 2021 hadi Aprili, 2021 lengo la makusanyo limefikiwa kwa zaidi ya asilimia 82.

“Mwezi Februari 2021, lengo la makusanyo lilifikiwa kwa silimia 82.9, Machi 2021, asilimia 84.1 na mwezi Aprili 2021, lilifikiwa kwa asilimia 83.2,” alifafanua Mhe. Dkt. Nchemba

Kuhusu akiba ya fedha za kigeni Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa hadi kufikia aprili 30, 2021, akiba ilikuwa dola za Marekani milioni 4,969.7 ambayo inatosha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 5.8 zaidi ya lengo la nchi la miezi 4 na pia zaidi ya lengo lililowekwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) la miezi 4.5.

No comments: