Habari za kifo cha Temitope Balogun Joshua ambaye ni maarufu kwa jina T.B Joshua zimewashangaza raia wengi wa Nigeria na dunia kwa ujumla.
Kanisa lake la Sinagogi la mataifa yote SCOAN ambalo lilianzishwa na muhubiri huyo lilithibitisha habari za kuhuzunisha za kifo chake Jumapili alfajiri likisema:.
Muhubiri TB Joshua anaacha sifa za huduma na kujitolea kwa ufalme wa Mungu ambao utaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo.
Wosia wa T.B Joshua
Muhubiri TB Joshua ni raia wa Nigeria kiongozi na mwanzilishi wa kanisa la SCOAN ambalo limekuwa likirusha matangazo yake mubashara katika runinga ya Emmanuel TV mjini Lagos kusini mwa Nigeria.
Alizaliwa kama Temitope Balogun Joshua mnamo tarehe 12 mwezi Juni ,1963 katika jimbo la Ondo nchini Nigeria.
Kulingana na Mtandao wa kanisa lake la SCOAN , Joshua alikuwa ndani ya tumbo la mamake kwa miezi 15 kabla ya kuzaliwa kwake.
Joshua alisomea katika shule ya msingi ya St. Stephen Anglican {Ikare-Akoko, Nigeria 1971-1977} lakini aliwacha shule alipojiunga na shule ya upili baada ya mwaka mmoja na kufanya kazi katika shamba moja la kuku.
Akiwa shuleni alijulikana kama muhubiri mdogo kutokana na alivyokuwa akiipenda Biblia na uwezo wa kutabiri matukio yaliofanyika katika jamii yake , kulingana na mtandao wa SCOAN.
Alianzisha kanisa la SCOAN mwaka 1987 akiwa na waumini wachache kabla ya kanisa hilo kupanuka hadi kimataifa.
Mwaka 2009 TB Joshua alianzisha klabu ya kandanda kwa jina My people FC katika juhudi za kuwasaidia vijana.
Wanachama wawili wa timu hiyo Sani Emmanuel na Ogenyi Onazi walichezea Nigeria Golden mwaka 2009, katika kombe la dunia la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17.
Tayari wachezaji watatu wamepata ufadhili Ulaya kuwa wachezaji wa kulipwa nchini Sweden.
Kulingana na jarida la Forbes 2011 , Temitope Joshua ni muhubiri wa tatu tajiri nchini Nigeria akiwa na thamani ya $15m.
Utata wa TB Joshua
Baadhi ya watu wamekuwa wakimkosoa kutokana na idadi ya miujiza yake anayofanya katika mikutano yake.
Baraza la makanisa ya Pentecostal nchini Nigeria PFN , chini ya mwavuli wa makanisa ya Pentecostal nchini Nigeria hayakubaliani na kanisa la muhubiri huyo wakimtaja TB Joshua kuwa kibaraka.
Christ Okote muhubiri wa kanisa maarufu nchini Nigeria alimshutumu Joshua kwa kuwa 'mganga'
Wakosoaji wake wa Kikristo wanasema kwamba mbinu zinazotumiwa na Joshua haziendani na zile za biblia.
Chanzo - BBC Swahili
No comments:
Post a Comment