Mwanafunzi aliyeuawa
***
JESHI la polisi mkoa wa Iringa linamshikilia mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa Prudence Patrick (21) mkazi wa Semtema Iringa kwa tuhuma za kumua kwa kumnyonga shingo mpenzi wake
Petronila Mwanisawa (22) mkazi wa Semtema kata ya Kihesa.
Mtuhumiwa wa mauaji ni mwenyeji wa mkoa wa Kagera na alikuwa ni mwanafunzi wa kozi ya uandishi wa habari na marehemu pia alikuwa ni mwanafunzi mwenzake na ni mwenyeji wa Sumbawanga.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Juma Bwire amewaeleza waandishi wa habari leo ofisini kwake kuwa tukio hilo limetokea majira ya 12 alfajiri katika eneo la Semtema kata ya kihesa Manispaa ya Iringa kwenye chumba alichokuwa akiishi mtuhumimiwa huyo.
Alisema kuwa marehemu alifika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo usiku wa kuamkia Juni 1 mwaka 2021 akiwa na rafiki yake aliyefahamika kwa jina la Belnada Njafula kwa lengo la kuchukua pesa yake kiasi cha Tsh 500 ambayo alikuwa anamdai mpenzi wake huyo.
" Baada ya kufika nyumbani kwa mtuhumiwa rafiki yake aliondoka na kuwaacha wawili hao kwa muda ili walipane deni walilokuwa wakidaiana, hata hivyo marehemu hakurudi nyumbani kwao hadi pale mwili wake ulipokutwa ndani ya chumba cha mtuhumiwa ukiwa umefungiwa ndani na umelazwa kitandani ukitokwa na povu mdomoni na damu puani" alisema kamanda Bwire .
Alisema taarifa za awali za kiuchunguzi zinaonesha mtuhumiwa baada ya kufanya unyama huo alitumia simu ya marehemu kutumiana ujumbe na rafiki yake kumjulisha kama ana mimba ya Jay ambaye ni rafiki yake.
"Mtuhumiwa alitumia simu ya marehemu kuchati na rafiki wa marehemu kumjulisha kuwa ana mimba ya Jay na baadae kuwajulisha wazazi wa marehemu kuwa binti yenu amefariki dunia",aliongeza
Kamanda Bwire alisema taarifa za awali kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo zilitolewa na wazazi wake kutokana na taarifa walizotumiwa na kijana huyo mtuhumiwa.
Alisema kuwa baada ya kufanya unyama huo mtuhumiwa huyo alikamatwa na jeshi la polisi akijaribu kutoroka kuelekea mkoani Dodoma na alikamatwa maeneo ya Mgongo kilomita chache kutoka maeneo ya Semtema alikofanya mauaji hayo.
Hata hivyo alisema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo unaendelea na pindi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
CHANZO - MATUKIO DAIMA BLOG
No comments:
Post a Comment