Samirah Yusuph.
Bariadi. Bodi ya pamba Tanzania (TCB) imewafikia wakulima 99,468 waliopo wilaya ya Bariadi katika kampeni ya kitaifa ya kuongeza tija ya kilimo cha pamba nchini .
Kampeni hiyo iliyozinduliwa wilayani hapo juma lililopita ikilenga kuwawezesha wakulima kupata uelewa wa vipimo sahihi na vyenye tija katika maandalizi ya kilimo cha pamba pamoja na upandaji wa mbegu.
Akizungumza na watendaji wa vijiji,kata, maafisa kilimo na ugani pamoja na wakuu wa idara katika wilaya ya Bariadi baada ya kukamilisha mafunzo barozi wa kilimo cha pamba nchini Agrey Mwanri amesisitiza kuendelea kutoa mafunzo ya mfumo bora wa kilimo cha pamba kwa wakati ili msimu wa kilimo unapo anza kila mkulima awe na uelewa wa kutosha.
Mwanri amesema kuwa ili kila mkulima tumie mfumo wa kisasa wa sentimita 60 kwa 30 ni lazima viongozi wote katika wilaya washiriki kikamilifu katika kutoa elimu kwa kuonyesha tija iliyopo iwapo mkulima atatumia mfumo huu wa vipimo pamoja na manufaa yake katika uzalishaji.
"Shirikiana na mkulima tangu hatua za awali muelimishe namna ya kuweka mbolea msimamie hadi mavuno na yeye akiwa anaona shamba lako la lake yote yapo sawa sio unaenda kumpangia masharti tayari anakaribia mavuno, tuanze nao tangu mwanzo".
Kwa upande wake Renatus Luneja Mkaguzi wa kutoka bodi ya Pamba alieleza kuwa pamoja na kuhamasisha matumizi ya samadi na mbolea za viwandani pia viongozi wananwajibu wa kuhakikisha wakulima wote wanakuwa katika vyama vya ushirika.
"Ni rahisi kuwafikia wakulima wanapokuwa Katika vyama vya ushirika hamasisheni wajiunge katika ushirika huku mkiendelea kuwapa elimu ili tija ya kilimo ionekane".
Kampeni ya kuongeza tija ya kilimo cha pamba nchini imelenga kuwafikia wakulima zaidi ya laki tano katika mkoa wa Simiyu ambapo hadi sasa zaidi ya wakulima laki moja wa wilaya ya Busega na Bariadi tayari wamefikiwa.
No comments:
Post a Comment