ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 5, 2021

WIZARA YA ELIMU KUJENGA MAABARA ZA MUDA KATIKA TAASISI YA SAYANSI ZA BAHARI YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM ZANZIBAR

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na viongozi Waandamizi wa chuo hicho wakikagua eneo zitakapojengwa maabara za muda za Taasisi ya Sayansi za Bahari katika kampasi ya Buyu.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa William William Anangisye akimuonesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako vifaa mbalimbali vya maabara za Taasisi ya Sayansi za Bahari vilivyoteketea kwa Moto.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe Profesa Joyce Ndalichako akiangalia uharibifu wa miundo mbinu ya maabara za Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zilizoteketea kwa moto Oktoba 2 , 2021 katika eneo la Mizingani Bandarini Zanzibar.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohamed Said pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe wakikagua Maabara za Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zilizoteketea kwa moto Jana Oktoba 4 , 2021 katika eneo la Mizingani Bandarini Zanzibar.

Na WyEST,Zanzibar

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako, amesema Wizara itahakikisha Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyoko Zanzibar inajengewa Maabara za muda na kuwekewa vifaa baada ya moto kuteketeza maabara zote na vifaa siku ya Jumamosi Oktoba 2, 2021 ili kuwezesha wanafunzi kuendelea na masomo watakapofungua chuo.

Akizungumza mjini Zanzibar Oktoba 4, 2021 baada ya kukagua uharibifu uliotokea kwenye jengo la maabara la Taasisi hiyo lililoko eneo la Mizingani Bandarini, Waziri Ndalichako amesema pamoja na kujenga maabara za muda Wizara ina mpango wa kujenga maabara za kudumu na kwamba tayari Serikali kupitia Wizara ilishatoa Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara mpya, hivyo ameagiza sehemu ya fedha hizo zitumike kununua vifaa muhimu vya maabara zitakazotumika kwa muda.

“Sisi kama Wizara tunaendelea kutekeleza kwa vitendo maono ya Mhe. Rais ya kuhakikisha elimu yetu inatoa vijana wenye ujuzi katika eneo hili la sayansi za bahari na ndio maana wiki iliyopita tumetoa kwa Taasisi hii Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha maabara mpya, hivyo pateni kibali cha kutumia sehemu ya fedha hizo kununua vifaa,” amefafania Waziri Ndalichako.

Aidha, Prof. Ndalichako amemuagiza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye kuhakikisha Chuo kinafunguliwa Oktoba 25, 2022 kama ilivyopangwa ili kutoathiri mzunguko wa Mwaka wa Masomo na kuwataka wanafunzi wa Chuo hicho kutokuwa na hofu .

Ndalichako ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jeshi la Polisi, Idara ya Zimamoto kikosi cha Bandarini na Kamisheni ya Maafa iliyoko chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar pamoja na Raia wema kwa kazi kubwa ya kudhibiti na kuzima moto huo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Simai Mohamed Said amemshukuru Prof. Ndalichako kwa kufika katika eneo hilo na kuahidi kushirikiana na chuo hicho kuhakikisha shughuli za Masomo zinaendelea kutokana na umuhimu wa Taasisi hiyo kwa uchumi wa nchi.

“Sote tunatambua umuhimu wa Taasisi hii ambayo ni chachu na kitovu cha kuimarisha uchumi wa Buluu na maabara hizi zilikuwa tegemeo si kwa Tanzania tu bali hata nchi za jirani hivyo tutashirikiana kuhakikisha zinarejea katika kipindi kifupi,” amesema mhe. Simai.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema moto huo ulizuka Jumamosi mchana katika jengo la maabara eneo la Mizingani Bandarini na kuteketeza maabara zote 3 pamoja na vifaa, vyumba vya madarasa 3, ofisi 2 na chumba cha “Server”.

Amesema Taasisi mbalimbali na jeshi la polisi zinaendelea na uchunguzi ili kubaini hasara halisi na kuongeza kuwa Chuo tayari kimeandaa mpango wa kuwezesha masomo kuendelea mara kipindi cha masomo kwa mwaka 2021/2022 kitakapoanza Oktoba 2021. Amesema mpango huo ni Pamoja na kujenga maabara za muda katika eneo la Buyu yalipo makao makuu ya Taasisi hiyo.

Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam iliyopo Zanzibar ina wanafunzi zaidi ya 100 wa Shahada ya Awali, Umahiri na Uzamivu kutoka Tanzania na nje ya Tanzania.

No comments: