ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 13, 2023

KAIRUKI AWATAKA WAKURUGENZI WA HALMASHAURI, WAGANGA WA MIKOA NA WILAYA KUONGEZA USIMAMIZI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki akifungua kikao kazi cha Waganga Wakuu na Waratibu wa UKIMWI wa Halmashauri kinachoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mount Meru.

Na James Mwanamyoto, OR- TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Wilaya na Waganga Wafawidhi wa vituo vya afya nchini kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa huduma za afya.

Mhe. Kairuki ametoa maelekezo hayo leo jijini Arusha alipokuwa akifungua kikao kazi cha watendaji hao wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waratibu wa UKIMWI na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kinacholenga kuongeza ufanisi kiutendaji.

Waziri Kairuki amewataka watendaji hao kuhakikisha fedha zilizotolewa na Serikali katika sekta ya afya zinatumika ipasavyo katika kuboresha huduma za afya nchini.

“Ni vema mkahakikisha kwamba vituo vyote vya kutolea huduma za afya vilivyokamilika vinaanza kutoa huduma ili kuwapunguzia gharama na adha wananchi ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma,” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Aidha, Mhe. Kairuki amesema moja ya kigezo kitakachotumika kupima utendaji kazi wa watendaji hao ni pamoja na kusimamia kikamilifu vituo vya afya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Kairuki amewataka watendaji hao kuhakikisha mifumo iliyopo ya kiutendaji inafanyakazi kwa ufanisi katika sekta ya afya ukiwepo Mfumo wa Dharula wa Rufaa wa M-Mama uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Mwezi Aprili 2022 ambao umepunguza vifo vya mama na mtoto, akitoa mfano kwa mkoa wa Shinganga ambao vifo kwa upande wa akina mama vimepungua kwa asilimia 38 na kwa watoto ni asilimia 45.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Denis Londo amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kuweka mkakati madhubuti wa kulinda na kuendelea kuboresha afya ya kila mtanzania.

Pia, Mhe. Londo amesisitiza uwajibikaji wa watendaji hao wa afya katika kusimamia miradi ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kutafuta fedha ili wananchi wanufaike na huduma za afya.

Awali, Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI anayeshugulikia Afya Dkt. Charles Mahera amesema kikao kazi hicho cha siku mbili kina lengo la kuwajengea uwezo wa kiutendaji na uelewa wa pamoja watendaji hao wa sekta afya katika utekelezaji wa utoaji wa huduma za afya katika ngazi ya msingi kwenye Halmashauri.

Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amewapongeza watendaji hao wa sekta ya afya kwa kuendelea kuwahudumia wananchi katika maeneo yao ya kazi.

No comments: