ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 23, 2023

KAMATI YA BUNGE YAMPONGEZA RAIS SAMIA KUBORESHA SEKTA YA AFYA NCHINI.


Na. Majid Abdulkarim, WAF, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutumia fedha za UVIKO kuboresha Sekta ya afya ili wananchi kupata huduma bora.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Taifa ya magonjwa ya afya ya akili Milembe na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Dkt. Ndungulile amesema kuwa, zaidi ya Bilioni 10 zimetumika kuboresha Sekta ya Afya ambapo katika hospitali ya Hospitali ya Taifa ya magonjwa ya afya ya akili Milembe wameona jengo la kisasa la wagomjwa wa dharula, jengo la wagonjwa maututi na mashine ya mionzi (X-RAY).

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wameweza kutembelea jengo la wagonjwa wa dharura pamoja na jengo la wagonjwa maututi na kuona Serikali ilivyoboresha maeneo hayo kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, ametoa wito kwa Wizara ya afya kuongeza nguvu zaidi katika huduma za afya ya akili kwani hivi karibuni matatizo hayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.

“Hivyo ili kuendana na kasi ya kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili nchini kuna haja ya ya kusogeza huduma za afya ya akili katika ngazi ya msingi ili kusaidia wananchi walipo katika maeneo ya kata, vijiji vyote katika majimbo yetu.” Amesema Dkt. Ndungulile.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ametoa rai kwa kamati hiyo kuwa na utamaduni wa kutembelea hospitali na taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara ya afya ili kushuhudia uwekezaji mkubwa uliofanyiwa na Serikali kwenye eneo la afya chini ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

No comments: