ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, June 13, 2023
MEJA JENERALI MBUGE -TUIMARISHE USHIRIKIANO KUKABILI MAJANGA
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.
Na Mwandishi Wetu- Singida
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuimarisha ushirikiano na sekta mbalimbali katika kukabiliana na maafa ili kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Singida na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja.
Meja Jenerali Mbuge amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la mwingiliano wa binadamu, wanyama na mazingira ambao husababisha kutokea kwa magonjwa mbalimbali yanayotoka kwa wanyama na kwenda kwa binadamu hivyo ipo haja ya kuwepo kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali katika kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na majanga hayo.
“Tunahuisha mwongozo huu kwa sababu ya mabadiliko ya sheria na kanuni za usimamizi wa Maafa. Mwongozo huu ni muhimu katika kurahisisha ushirikiano wa kisekta ili kujenga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya milipuko ya magonjwa na dharura zingine zenye madhara kwa afya ya binadamu, wanyama na mazingira,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa husisitiza yakiwemo Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Wanyama (WOAH) na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) kwa pamoja husisitiza ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kuwa na mikakati na sera za pamoja katika kuimarisha afya ya wanadamu, wanyama na mazingira.
“Ili kutekeleza dhana ya Afya moja, ni muhimu kuwa na miongozo mbalimbali ili kurahishisha uratibu na utendaji katika ngazi zote. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru FAO ambao walianzisha mchakato wa kutengeneza mwongozo huu ambao katika kikao hiki utauhuishwa na kutafsiriwa,” ameeleza.
Aidha amebainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Menejimenti ya Maafa ina wajibu wa kuratibu utekelezaji wa dhana ya Afya Moja kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya 2004, Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 pamoja na Mkakati wa Afya Moja 2022-2027.
Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Valentina Sanga akiwasilisha Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja .
Mtaalam wa Afya ya Jamii kutoka Shirika la Afya Duniani Bi. Pelagia Muchuruza akieleza jambo wakati wa kikao hicho.
Afisa Kiungo wa Afya Moja kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Justine Assenga akifafanua jambo katika kikao hicho.
Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.
Baadhi ya Wataalam kutoka sekta mbalimbali wakifuatilia kikao kazi cha Watalam waliokutana kwa lengo la Kuhuisha na Kutafsiri Mwongozo wa Utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja mkoani Singida.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment