ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 12, 2023

NYAMA YA TANZANIA KUANZA KUUZWA NCHINI MISRI


Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Taifa ya Huduma za Miradi (NSPO) Meja Jenerali, Hossam Nigeda (kulia) akimkabidhi Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega barua ya mualiko wa kwenda nchini misri kwa ajili ya kwenda kuona shughuli za sekta ya mifugo na uvuvi zinavyotekelezwa nchini humo. Tukio hilo lilifanyika wakati wa kikao kifupi cha asubuhi "Breakfast Meeting" kilichofanyika jijini Dodoma mapema leo Juni 12, 2023
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Ujumbe kutoka nchini Misri ulioongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Taifa ya Huduma za Miradi (NSPO) Meja Jenerali, Hossam Nigeda (kushoto kwake) wakati wa kikao kifupi cha asubuhi "Breakfast Meeting" kilichofanyika jijini Dodoma mapema leo Juni 12, 2023.


Na Mbaraka Kambona
Nyama ya Tanzania kuanza kuuzwa nchini Misri baada ya ujumbe kutoka nchini humo kukutana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na kumueleza kuwa lengo lao kabla ya Sikukuu ya Eid al Hajj waanze kusafirisha tani mia moja (100) za nyama ili kuanza kutangaza soko la nyama kutoka Tanzania.

Hayo yalifahamika wakati wa kikao kifupi cha asubuhi "Breakfast Meeting" kilichofanyika jijini Dodoma mapema leo Juni 12, 2023 baina ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega na Ujumbe kutoka nchini Misri ulioongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Taifa ya Huduma za Miradi (NSPO) Meja Jenerali, Hossam Nigeda.

Katika mazungumzo yao, Meja Generali, Nigeda alimueleza Mhe. Ulega kuwa lengo lao ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili kwa kufungua soko la nyama ya Tanzania nchini Misri.

Aliongeza kuwa wamejipanga kuanzisha machinjio ya kisasa hapa nchini ambayo itawawezesha kusafirisha Tani Mia Sita (600) ya nyama kila Mwezi, pia kusafirisha wanyama hai wakiwemo ng'ombe, Kondoo na Mbuzi Elfu Kumi (10,000) kila Mwezi.

Alifafanua kuwa kwa siku za hivi karibuni wapo katika mipango ya kusafirisha Tani Mia Moja (100) za nyama kabla ya sikukuu ya Eid Al Hajj ili kuanza kutangaza soko la nyama ya Tanzania nchini humo.

Misri ni miongoni mwa nchi zenye Idadi kubwa ya watu barani Afrika ambapo Idadi ya watu wake hawapungui Milioni 120 hivyo itakuwa fursa nzuri ya kibiashara kwa Tanzania hususan biashara ya nyama.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alimuhakikishia Meja Jenerali Nigeda kuwa Tanzania ipo tayari na watawapa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha biashara hiyo iweze kuanza haraka iwezekanavyo.

Wajumbe wengine waliombatana na Meja Jenerali Nigeda ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Taifa ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji, Islam Attia Abdel Hamid, Mwenyekiti wa Huduma za Mifugo, Misri, Meja Jenerali, Dkt. Ihab Saber Youssef na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Masr Trading, Dkt. Hatem Ahmed.

Ziara hiyo ni miongoni mwa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kufungua milango ya kibiashara nje ya nchi.

No comments: