Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali bungeni, jijini Dodoma.
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imeeleza kuwa imekamilisha usanifu wa Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (One Stop Boarder Post- OSBP) Manyovu kilichopo mkoani Kigoma na ujenzi upo kwenye taratibu za awali za kumpata mkandarasi.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Buhigwe, Mhe. Kavejuru Felix, aliyeuliza Serikali itaanza lini ujenzi wa Kituo cha Forodha cha Manyovu.
Akieleza kuhusu fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa Kituo hicho, Mhe. Chande alisema kuwa Serikali ipo katika hatua ya uchambuzi wa fidia na utaratibu utakapokamilika wananchi watapata haki yao.
Kwa upande mwingine akijibu swali, kuhusu mchango wa Mkoa wa Kagera kwenye pato la Taifa, alisema kuwa kwa mujibu wa Taarifa ya National Accounts for Tanzania Mainland inayoandaliwa na kusambazwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, hadi kufikia mwaka 2021, Mkoa wa Kagera ulichangia asilimia 2.6 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 2.5 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2020.
“Serikali imeweka mazingira wezeshi ili wananchi wenyewe waweze kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii zitakazowaongezea kipato chao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla”, alisema Mhe. Chande.
Alisema kuwa Serikali imefanya jitihada za kimkakati ambapo imeweka nguvu katika maeneo ya uzalishaji hususani kwenye kilimo cha umwagiliaji, mifugo na uvuvi ili kuinua uchumi kwa haraka.
No comments:
Post a Comment