Na John Walter-Arusha
Mzee Laxford Kajuna mkazi wa Njiro jijini Arusha amejikuta akitokwa na machozi mara baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa kufika katika eneo lake na kuzuia kufutiwa umiliki wa eneo hilo ambalo amekuwa akilitumia kwa ufugaji wa nguruwe.
Mzee Kajuna amekuwa akilalamikiwa na majirani zake kwa kufanya shughuli ya ufugaji wa nguruwe zaidi ya 5,000 katika eneo la makazi, jambo ambalo limekuwa kero kwa majirani zake.
Waziri Silaa amefika katika makazi ya mzee huyo na kukuta shughuli ya ufugaji huo ukiendelea licha ya kupewa notisi ya siku 30 ya kuhamisha mifugo yake kutoka Ofisi ya Halmashauri ya jiji la Arusha.
Awali Mzee Kajunaalimilikishwa eneo hilo kwa matumizi ya makazi na biashara na badala yake amekuwa akilitumia kwa ufugaji wa nguruwe ambao wamekuwa kero kwa majirani zake kutokana na harufu, sauti za mifugo na uchafu wa mazingira ya mifugo hao.
Mara baada ya kuchukua muda mrefu kwa Mzee kajuna kutekeleza notisi hiyo ya siku 30 ya kuhamisha mifugo hiyo, alipewa notisi nyingine ya pili ya kubatilishwa umiliki wa eneo hilo kwa kuwa amekiuka matumizi ya eneo lake.
Katika kulitatua suala hilo Waziri Silaa amempa muda wa kutosha wa kuhamisha mifugo yake taratibu mara baada ya kukatika kwa mvua za msimu huu ambazo zimeonekana ni kikwazo kwa uhamishaji wa mifugo hiyo.
Aidha, Waziri Silaa amemhurumia mzee Kajuna kutobatilishiwa matumizi ya eneo hilo ambalo alikuwa anyang'anywe kwa kufanya shughuli ya ufugaji eneo la makazi na bishara.
Hata hivyo, Mzee Kajuna ameanza kuhamisha mifugo yake na hadi sasa ameisha hamisha nguruwe 1,500 ambapo tayari amepata eneo wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
No comments:
Post a Comment