Monday, February 26, 2024

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI AKAGUA UKARABATI NA UPANUZI WA KIWANJA CHA NDEGE SONGEA


Naibu waziri wa uchukuzi David Kihenzie kulia,akimsikiliza meneja wa kiwanja cha ndege cha Songea Mhandisi Danstan Komba, wakati alipotembelea kiwanja hicho kukagua ili kujionea kazi ya ukarabati na upanuzi iliyofanywa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 37.

Na Muhidin Amri, Songea
NAIBU Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile,ameugiza uongozi wa mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania(TCAA),kuvunja haraka mkataba na kampuni ya Manyanya Engineering Company Ltd inayokarabati jengo la abiria katika kiwanja cha ndege cha Songea mkoani Ruvuma.

Ametoa agizo hilo jana, mara baada ya kukagua kiwanja cha ndege cha Songea kilichofanyiwa upanuzi na ukarabati mkubwa na serikali ya awamu ya sita kwa gharama ya Sh.bilioni 37.

Alisema,ni vyema mamlaka hiyo kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi huyo ambaye anafanya kazi hiyo kwa kusua sua licha ya serikali kutoa cha Sh.milioni 423 kwa ajili ya kazi hiyo.

Kwa mujibu wa Naibu waziri Kihenzile ni kwamba,kampuni ya Manyanya ilitakiwa kukamilisha kazi tangu mwezi Novemba 2023 lakini hadi sasa kazi iliyofanyika ni asilimia 30 tu na yuko nyuma ya mkataba kwa zaidi ya miezi mitatu.

Aidha,ameagiza atafutwe mkandarasi mwingine mwenye uwezo ili jengo hilo liweze kukamilika haraka kwa ajili ya abiria wanaotaka kusafiri kwenda nje na wanaokuja katika mkoani Ruvuma kwa shughuli mbalimbali zikiwemo biashara na utalii.

“watu wanaopewa kazi alafu hawakamilishi, lawana haziendi kwao bali zinakwenda kwa mkuu wa nchi Mheshimiwa Rais ambaye anadhamira njema na wananchi wake”alisema.
Sambamba na hilo,ameitaka mamlaka hiyo kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo kubwa la abiria katika kiwanja hicho linaloendana na ukubwa na adhi ya mkoa wa Ruvuma.

Alisema,kiwanja cha ndege cha Songea ni cha Kihistoria na kiwanja cha mkakati kilichojengwa kwa mara ya kwanza mwaka 1974 na kukamilika mwaka 1980 na tangu wakati huo hakijawahi kufanyiwa ukarabati wala matengenezo.

Kihenzile,amewataka watumishi wa viwanja vingine vya ndege hapa nchini,kuiga utendaji kazi wa meneja wa kiwanja cha ndege Songea Mhandisi Danstan Komba aliyehakikisha kiwanja hicho kimepata hati ya umiliki wake.

Amewaomba wananchi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine hapa nchini,kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye katika kipindi cha uongozi wake amefanya mambo mengi makubwa kwa wananchi wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.

Amewasisitiza watumishi wa kiwanja wa viwanja vya ndege nchini kuchapa kazi,kwa uadilifu na kuwa waaminifu na kuhakikisha wanatoa huduma bora ili kuwavutia wateja kusafiri kwa kutumia ndege za shirika la ndege Tanzania(ATCL) na ndege za mashirika mengine.

Meneja wa kiwanja cha ndege cha Songea Mhandisi Danstan Komba alisema,serikali kupitia wizara ya uchukuzi imetekeleza mradi wa upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha hicho.

Alisema,lengo kubwa ni kuboresha miundombinu kwa ajili ya kuwezesha ndege aina ya Bombadier Q-400 au ATR 72 yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 70 kutumia kiwanja hicho.

Alitaja kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kufanya matengenezo ya sehemu ya kuruka na kutua ndege kutoka mita 1,600 hadi kufikia mita 1,860,kujenga mnara wa kuongoza ndege,kufunga taa,kujenga uzio kuzunguka uwanja kazi ambazo zimekamilika kwa asilimia 100.

Komba alitaja kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa Barabara ya ndege,Barabara ya kiungio,kujenga sehemu ya maegesho ya ndege na kujenga kituo cha nishati.

Kwa mujibu wa Komba,katika kuhakikisha kuwa kiwanja hicho kinaendelea kutoa huduma wezeshi na tosherezi,mamlaka imechukua hatua ya kubadili matumizi ya jengo la mhandisi mshauri ili litumike kuhudumia abiria ambalo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 145 kwa wakati mmoja.

Katika hatua nyingine Komba alisema, kwa sasa kiwanja hicho kinatoa huduma kwa ndege ya ratiba na ndege za dharura na kwa sasa kuna shirika moja tu la ndege la ATCL.

Katika hatua nyingine Komba alisema, katika kipindi cha miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2019-2024 miruko ya ndege imeongezeka kutoka 304 hadi kufikia miruko 468 mwaka 2023.

Pia alieleza kuwa hata idadi ya abiria imeongezeka kutoka 2,025 mwaka 2019 na kufikia 18,580 mwezi Disemba 2023.

Mkuu wa wilaya ya Songea Kapenjama Ndile alisema, kwa sasa kiwanja hicho ni muhimu kwa kuwa kinatumika na wananchi wa mikoa mingine jirani ya ukiwemo mkoa wa Njombe.


No comments: