Advertisements

Monday, February 12, 2024

WAKAZI MALOLO WAMKATAA HAKIMU ALIYEKAA MUDA MREFU


Mbunge wa Jimbo la Mikumi Denis Londo akiongea na wananchi wa kata ya Malolo Wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro
Na Christina Cosmas, Morogoro


WAKAZI wa Kata ya Malolo Tarafa ya Mikumi Wilayani Kilosa mkoani Morogoro wamemkataa Hakimu wa eneo hilo kwa kile wanachodai kuwa ni amekaa muda mrefu huku akionesha kupenda rushwa.

Wakazi hao wamesema hayo jana mbele ya Mbunge wa Jimbo la Mikumi Wilayani Kilosa Denis Londo alipofika katika kata hiyo kukabdhi gari la wagonjwa ili kunusuru vifo vya watu hasa wajawazito na watoto wachanga wanapokwenda kupata huduma.

Mmoja wa wakazi wa Malolo Mgonela Kibiki anasema akiwa mkazi wa muda mrefu kwenye kata hiyo anashangazwa na Serikali kuendelea kumbakiza Hakimu huyo aliyekaa kwa zaidi ya miaka 25 kwenye kata hiyo na hivyo kujenga mazoea na kutokuwa mtendaji mzuri wa kazi zake.

Mgonela anasema ni vema hakimu huyo akahamishwa kwa sababu anashindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo ambapo yeye aliwahi kupeleka kesi yake ya madai na mdaiwa kutakiwa kuwasilisha fedha kwa hakimu ili yeye akachukue na hakimu huyo kutomlipa zaidi ya shilingi Milioni moja licha ya kuwa tayari amepokea.

Akijibu tuhuma hizo Mbunge wa jimbo la Mikumi Denis Lazaro Londo alikiri kutokuwepo kwa sheria inayoruhusu kiongozi yoyote kukaa muda mrefu sehemu moja.

Mbunge Londo aliahidi kulifikisha suala hilo kwenye vyombo husika ili liweze kufanyiwa kazi mara moja.

No comments: