Nchi ya Iran imerusha ndege za kivita zisizo na rubani (UAVs) zaidi ya 50 kwa ajili ya kwenda kuishambulia Israel ambazo kwa sasa zipo angani na zimeshapita anga la Iraq kwa kasi zikielekea Israel , Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limethibitisha na kusema tayari limechukua tahadhari zote ili kudhibiti ndege hizo zisilete madhara.
Jeshi la Israel limesema limejipanga kwa vita likiwa tayari na ndege za kivita na meli za kivita ambazo zinalinda mashambulizi ya angani na majini kutoka Iran.
Iran imefanya mashambulizi hayo ya drones za kivita licha ya onyo la Rais wa Marekani, Joe Biden alilolitoa jana akiitaka Iran isiishambulie Israel ambapo alisema Marekani itasaidia kuilinda Israel na Iran haitofanikiwa kuishambulia ikisema lengo la Marekani ni kuepusha ugomvi kuwa mkubwa.
Marekani ilipeleka meli zake pamoja na vikosi vya kijeshi kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati kwa ajili ya kuilinda Israel, ikitarajia kuyatengua mashambulizi yoyote ya moja kwa moja kutoka Iran dhidi ya Israel, ambayo yalishahisiwa kuwa yatafanyika Ijumaa au Jumamosi.
Hatua ya Iran kuishambulia Israel inakuja kama sehemu ya kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi dhidi ya Ubalozi mdogo wa Iran Mjini Damascus, Syria, Wiki iliyopita, mashambuli hayo ambayo Iran na Marekani zinaamini yalifanywa na Israel, yaliwaua Watu wanane, miongoni mwao akiwamo Kamanda wa ngazi za juu wa Kikosi Maalum cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran anayesimamia vikosi vya nje vya Quds na kama ambavyo imekuwa ikifanya kwenye mashambulizi mengine huko nyuma, kwenye mashambulizi haya ya Aprili Mosi, Israel pia haikusema kuwa ilihusika wala kukanusha.
Viongozi wa juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akiwamo Kiongozi Mkuu Ayatullah Ali Khamenei, walisema Israel lazima iadhibiwe na itaadhibiwa kwa mashambulizi hayo ambayo alisema yalikuwa sawa na kuishambulia Iran.
No comments:
Post a Comment