Monday, April 29, 2024

MAWAZIRI WA AFRIKA KUJADILI VIPAUMBELE VYA AFRIKA IDA 21


Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), akipokelewa na Waziri wa Fedha wa Kenya Prof. Njuguna Ndung’u, alipowasili kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uchangiaji wa Mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki ya Dunia (IDA21) ngazi ya Mawaziri, unaofanyika tarehe 28 Aprili mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, Jijini Nairobi, Kenya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El Maamry Mwamba, (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Kenya Dk. Chriss Kiptoo, kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uchangiaji wa Mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki ya Dunia (IDA21) ngazi ya Mawaziri, unaofanyika tarehe 28 Aprili mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, Jijini Nairobi, Kenya.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), akisalimiana na Waziri wa Mipango Angola Victor Hugo Guiherme, kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uchangiaji wa Mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki ya Dunia (IDA21) ngazi ya Mawaziri, unaofanyika tarehe 28 Aprili mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, jijini Nairobi, Kenya.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), akiteta jambo na Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini Enoch Godogwana, kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uchangiaji wa Mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki ya Dunia (IDA21) ngazi ya Mawaziri, unaofanyika tarehe 28 Aprili mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, Jijini Nairobi, Kenya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, na Kamishna wa Fedha za Nje Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Yussuf Ibrahim Yussuf (katikati) na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Noel Kaganda, wakiwasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uchangiaji wa Mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki ya Dunia (IDA21) ngazi ya Mawaziri, unaofanyika tarehe 28 Aprili mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, jijini Nairobi, Kenya.

Na. Josephine Majura na Saidina Msangi, WF, Nairobi, Kenya

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), ameungana na Mawaziri wa Fedha wa Afrika kushiriki katika mkutano maalum wa kujadili vipaumbele vya Afrika ili viweze kuzingatiwa katika maandalizi ya Mzunguko wa 21 wa Mfuko wa Maaalumu wa Maendeleo wa Benki ya Dunia (IDA21) unaotarajiwa kuanza Julai 2025 – Juni 2028.

Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, Jijini Nairobi, Kenya. ni utangulizi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Uchangiaji wa Mzunguko wa 21, utakaofanyika tarehe 29 Aprili mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano huo Dkt. Nchemba, alisema kuwa Tanzania imeungana na Mawaziri wengine katika kuhakikisha kuwa inasisitiza umuhimu wa kuongezewa fedha za dirisha la 21 la IDA ili kuweza kuchangia katika utekelezaji wa ajenda na malengo ya maendeleo ya Bara la Afrika.

“Hili dirisha limekuwa likitoa mikopo kwa masharti nafuu, riba kwa kiwango cha chini na muda wake wa kurudisha umekua mrefu ambapo Tanzania kwa kiwango kikubwa imekuwa ikitumia dirisha hilo kupata fedha ambazo zimekua zikitumika katika kuendeleza sekta za huduma za jamii kama vile elimu, maji pamoja na umeme kwa bei nafuu”, alisema Dkt. Nchemba.

Alifafanua kuwa dirisha hilo ambalo riba ya mikopo yake haizidi asilimia mbili limekuwa likitoa mikopo kwa nchi za Afrika yenye masharti nafuu ili kuzipunguzia nchi hizo kupata mikopo kutoka benki za kibiashara ambayo huwa na gharama kubwa.

Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa mkutano huo utasisitiza umuhimu wa kupatikana kwa fedha za IDA kwa ajili ya kuzisaidia nchi kutoka katika athari za majanga na kuwezesha kurejea katika hali ya kawaida kwa ajili ya maendeleo endelevu Afrika.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El Maamry Mwamba, Kamishna wa Fedha za Nje Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Yussuf Ibrahim Yussuf na viongozi wengine wa Wizara.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake