Sunday, May 26, 2024

CDE. MBETO : AMTAKA JUSSA KUACHA SIASA ZA KIHARAKATI


KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, akizungumza katika moja ya mkutano wa Vyombo vya Habari uliofanyika hivi karibuni.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis, amewataka viongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo kuacha upotoshaji juu ya mchakato wa zabuni za makampuni ya uingizaji wa mafuta nchini kwani kampuni ya GBP ndio iliyokidhi vigezo na kupewa tenda hiyo kwa mujibu wa sheria.

Alisema mchakato huo ulikuwa wazi kwa kampuni yoyote iliyokuwa na uwezo wa kuingiza mafuta itimize masharti mbalimbali yakiwemo kutoa huduma hiyo kwa wakati wote pia kulipwa fedha kidogo kidogo na wakati mwingine kwa mkopo vigezo ambavyo makampuni zaidi ya matano yalikataa kwa kudai kuwa yanahitaji kulipwa fedha taslimu kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani, vigezo ambavyo kampuni GBP ilikubali kutekeleza.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akitoa ufafanuzi juu ya upotoshaji huo uliotolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar Ismail Jussa wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa chama hicho Mkoa wa Kusini Unguja, aliyedai kuwa mikataba mingi mibovu inayogharimu nchi.

Katika madai ya Jussa, alisema katika zabuni ya kuingiza mafuta ya kampuni tano zilizoomba zabuni ya kuingiza mafuta ,iliyopendekeza zabuni kubwa ndio iliyopewa na kuachwa zilizopendekeza zabuni ndogo.

Mbeto, amefafanua kuwa kauli zilizotolewa na Jussa ni upotoshaji ukweli ni kwamba, Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, imeendelea kufanya juhudi kubwa za kuhakikisha inafunga mikataba halali na yenye maslahi mapana ya nchi.

“ Nishati ya Mafuta ni uti wa mgongo wa nchi inapokosekana kwa dakika moja sote tunajua hali inavyokuwa Zanzibar , kwani watu wanaangaika na hawafanyi kazi kwa ufanisi kwani wanaangaika kila kituo cha kutoa huduma hiyo kupata mafuta kwa ajili ya matumizi ya mashine,magari, na pikipiki.

Serikali haiwezi kuacha watu wakiangaika kwa kuwaendekeza makampuni yanayojali faida na kuweka mbele maslahi ya fedha badala ya maslahi ya nchini kwani kampuni ya GBP imejitolea kusambaza mafuta zaidi ya mwaka sasa wakilipwa fedha kidogo kidogo huku kampuni nyingine zikishindwa masharti ya kutoa huduma hiyo.”, alifafanua na kuwataka Viongozi wa ACT-Wazalendo kufanya utafti kabla ya kutoa kauli za upotoshaji.

Alisema Serikali imeyadhamini kampuni ya ndani yanayofanya biashara ya Mafuta ili kampuni ya GBP iendelee kuleta nishati hiyo ambapo kwa sasa inadai zaidi ya Bilioni 200.

Alifafanua kuwa hata makampuni ya ndani uwezo wao wa mitaji umeyumba kutokana na bei ya mafuta kupanda Duniani inayosababishwa na uwepo wa vita vya Urusi na Ukraine, matatizo ya nchi za mashariki ya kati, nchi za umoja wa Opec kupunguza uzalishaji kutokana na kupanda kwa Dola ya Kimarekani.

Katibu huyo wa NEC Mbeto, alisema makampuni yanayolalamika kutopewa tenda hiyo mengi hayana mtaji wa kutosha katika kuleta mafuta ya kukidhi soko la Zanzibar, hivyo wasitumie baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaofanya siasa za kiharakati kupandikiza mbegu za chuki kwa wananchi na kuharibu hadhi ya nchi katika soko la kikanda na kimataifa.

Pamoja na hayo alieleza kuwa kinachofanywa na viongozi wa Chama Cha ACT- Wazalendo ni kutafuta huruma ya wananchi na kutafuta umaarufu wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kufanya uchochezi na siasa za porojo zisizokuwa na ushahidi.

Aliwasihi wananchi kuendelea kuamini na kuunga mkono serikali iliyopo madarani kwani inafanya juhudi kubwa za kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora na yenye hadhi.

Sambamba na hayo Mbeto, alisema Zanzibar inahitaji kuwa vyama vya upinzani imara vyenye viongozi wenye maono na fikra za kujenga hoja zenye mashiko, kukosoa, kufanya utafti na kusimamia dhana ya uzalendo na utaifa sio kuwa madalali wa kisiasa.

Kampuni ya Gulf Bulk Petroleum (GBP) inajihusisha na biashara ya usafirishaji na uingizaji wa nishati ya mafuta ya petrol,dizeli, mafuta ya taa na mafuta ya ndege.



No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake