Sunday, May 26, 2024

DK. MOLLEL AONYA JAMII DHIDI YA MATUMIZI HOLELA YA ANTIBIOTIKI


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akizungumza kabla ya kuzindua Kampeni ya kupambana na usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa na Magonjwa ya Zuonotiki ulifanyika Tarehe 25 Mei, 2024 Jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu -Dar es Salaam.
Katika kuhakikisha Nchi inakuwa stahimilivu dhidi ya Maafa, Serikali imeweka utaratibu wa kushughulikia masuala ya Maafa kwa kutunga Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, pamoja na nyenzo nyingine ambapo Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 inatambua dhana ya Afya Moja ambayo inawezesha Sekta mbalimbali kushirikiana na kuwasiliana ili kudhibiti majanga ya Kiafya ikiwemo magonjwa ya zuonotiki na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya Dawa.
Akizungumza tarehe 25 Mei, 2024 Jijini Dar es Salaam kabla ya kuzindua kampeni ya kupambana na usugu wa Vimelea vya Magonjwa dhidi ya Dawa (UVIDA) na Magonjwa ya Zuonotiki kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema zipo sababu nyingi zinazochangia kuongezeka kwa usugu wa vimelea dhidi ya Dawa Nchini na kubwa ni tabia zetu za kila siku ikiwemo matumizi holela ya Dawa hizo.

“Matumizi holela ya dawa ni tabia ya Mgonjwa au mfugaji kununua au kutumia dawa bila kupata ushauri wa wataalamu pia Mgonjwa kutokumaliza dozi ya dawa kama ilivyoelekezwa wakati wa matibabu au Kutumia dawa zisizo na ubora au kuisha muda wake wa matumizi na matumizi ya antibayotiki kwenye chakula cha mifugo kwa ajili ya kunenepesha au kuharakisha ukuaji na baadaye pamoja na kula mazao ya mnyama yaliyotolewa bila kuzingatia muda wa kuisha dawa mwilini na utupaji wa masalia ya dawa kwenye mazingira yetu huchangia kuongezeka kwa tatizo la UVIDA”.Alisema Dkt. Mollel
Aidha Dkt. Mollel amesema kwa kuwa vimelea sugu vya magonjwa dhidi ya dawa vinaweza kuenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine na hivyo kuwa na uwezekano wa kuwa na janga kubwa la dawa kutokufanya kazi.
Aliongezea kuwa ni jukumu la kila mmoja kutoa mchango katika kuzuia UVIDA kwa kufika kwenye kituo cha kutolea huduma za afya endapo unaona dalili yoyote ya ugonjwa ili uweze kupewa matibabu sahihi, hii ni sambamba na ukamilishaji wa dozi kama ulivyoshauriwa na wataalam.

“Endapo wewe ni mfugaji, mnyama wako anapoumwa muone mtaalamu wa mifugo na fuata maelekezo ya kitabibu uliyopewa hii ni pamoja na kutokuuza mazao yatokanayo na mifugo hao kama maziwa, mayai na nyama kabla ya muda wa kusubiri kuisha”.Aliongeza Dkt. Mollel

Dkt. Mollel ametoa rai kwa jamii, Wizara, Idara na Taasisi za Umma, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha shughuli zote za maendeleo zinazingatia ushirikishwaji kwa maslahi mapana ya Nchi.




No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake