Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), linawaita vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita kwa mwaka 2024 kutoka shule zote za Tanzania bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2024.
Hayo yamesemwa leo Mei 24, 2024 na mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena, akifafanua kuwa pamoja na wito huo, JKT limewapangia makambi watakao kwenda kupatiwa mafunzo na wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia tarehe 01 Juni hadi 07 Juni 2024.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha vijana kujengewa uzalendo, umoja wa kitaifa, kufundishwa stadi za kazi na maisha pamoja na utayari wa kulijenga na kulitumikia taifa.
Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana hao wamepangwa katika kambi tofauti ikiwemo kambi za JKT Rwamkoma - Mara, JKT Msange - Tabora, JKT Ruvu - Pwani, JKT Mpwapwa, Makutupora JKT - Dodoma, JKT Mafinga - Iringa, JKT Mlale - Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba - Tanga, JKT Makuyuni - Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila - Kigoma, JKT Itaka - Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa - Rukwa, JKT Nachingwea - Lindi, JKT Kibiti- Pwani pamoja na Oljoro JKT- Arusha.
“Orodha kamili ya majina ya vijana hao, makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo makambi hayo yalipo na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo, inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz,”
Na kuongeza kuwa, “majina hayo pia yanapatikana kupitia simu ya mkononi, kwa mtumiaji kupiga USSD CODE *152*00#, kisha atachagua namba 8 (Elimu) ikifuatia na No 5 (JKT), ambapo mtumiaji ataingiza namba ya shule aliyosoma ikifuatiwa na majina yake matatu kisha mtumiaji ataoneshwa kambi alilopangiwa na mahali ilipo.”
Amesema huduma hiyo inapatakana kwa watumiaji wa mitandao yote ya simu nchini huku akiwataka vijana hao kuripoti wakiwa na vifaa watakavyotumia kambini ikiwa ni bukta ya rangi ya 'Dark Blue' yenye mpira kiunoni iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini, isiyo na zipu , t-shirt ya rangi ya kijani (Green Vest), raba za michezo zenye rangi ya kijani au blue, shuka mbili za kulalia zenye rangi ya blue bahari, soksi ndefu za rangi nyeusi, nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi, track suit ya rangi ya kijani au blue, nyaraka zote zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu zikiwemo vyeti vya kuzaliwa, uhitimu kidato cha 4 pamoja na nauli ya kwenda makambini na kurudi nyumbani.
Aidha Brigedia Jenerali Hassan Mabena ameongeza kuwa maandalizi ya kupokea vijana hao katika kambi mbalimbali yamekamilika kwani serikali imeendelea kuliwezesha jeshi hilo katika nyanja mbalimbali iliwemo fedha za maendeleo ambazo zimeboresha makambi katika mahanga pamoja na maeneo kwaajili ya kufanyia mafunzo hayo ya muda wa miezi mitatu.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake