Tuesday, May 21, 2024

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR AHUTUBIA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA NYUKI DUNIANI



Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Leo Jumatatu Mei 20, 2024, ameshiriki akiwa Mgeni Rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, huko Pujini Lima-anda, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Hafla hiyo imeandaliwa na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, kupitia Idara yake ya Misitu, kwa kushirikiana pia na Jumuiya za Wafugaji nyuki hapa Nchini, ZABA na PEBA.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu, ambayo yamefanyika katika Kanda na Mataifa mbali mbali Duniani, ni "NYUKI NA VIJANA".
Viongozi mbali mbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Wakurugenzi, Maafisa Wadhamini, Wafugaji wa Nyuki, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wawakilishi wa Jumuiya na Mashirika, Asasi za Kiraia, pamoja na Wananchi, wamehudhuria katika hafla hiyo wakiongozwa na Waziri sambamba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Mhe. Shamata Shaame Khamis, na Mhe. Ali Khamis Juma; Mkuu wa Wilaya ya Chake- Chake, Mhe. Abdallah Rashid Ali; Mkurugenzi wa Misitu, Ndg. Said Juma Ali; na Wakuu wa Chama cha ACT-Wazalendo wa Mikoa yote ya kichama, kisiwani Pemba.

Hafla hiyo ambayo imeanza na kukamilisha kwa Dua na Qur-an Tukufu, imeshuhudia harakati mbali mbali pamoja na Burudani, ikiwemo ya Utenzi kutoka kwa Vijana, Asma na Aziza Said Hamad.

Pamoja na Hatua hiyo, Mheshimiwa Othman amekagua Maonyesho ya Bidhaa za Wajasiriamali zinazotokana na Mazao ya Nyuki; kabla ya Kuongoza Zoezi la Kukabidhi Vifaa na Vitendea-Kazi kwa Wananchi na Vikundi mbali mbali vya Ufugaji, kutoka kwa Wadau wa Maendeleo, pamoja na 'BEVAC' Mradi wa Kuongeza Thamani ya Mazao ya Nyuki (Bee-keeping Value Addition Chain).
Mheshimiwa Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, amewasili kisiwani Pemba, kwaajili ya Ziara ya Siku Mbili, inayojumuisha Shughuli za Kiserikali na Chama.

Kitengo cha Habari. Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.





No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake