Na Fauzia Mussa. Maelezo. 14.05.2024.
Waandishi wa Habari nchini wameshauriwa kuandika habari za michezo na jinsia ili kuweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii juu ya dhana ya michezo na jinsia.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (Tamwa) ofisi ya Zanzibar Dkt. Mzuri Issa wakati alipokuwa akizungumza na jopo la Waandishi wa habari za jinsia na michezo huko Tunguu Mkoa wa kusini Unguja.
Amesema masuala ya michezo kwa wanawake yamekuwa hayazungumzwi ipasavyo jambo ambalo linapelekea kukosa fursa mbalimbali zinazotokana na michezo ikiwemo afya, ajira na kipato.
Aidha amewataka Wananchi kuachana na dhana potofu ya kuwa, Wanawake kushiriki katika michezo ni uhuni jambo ambalo halina ukweli ndani yake.
Hata hivyo aliwataka waandishi hao, kuutumia ipasavyo mradi wa maendeleo ya Michezo Afrika ili kuleta mabadiliko katika jamii na kufikia hatua ya wanawake na wasichana kuweze kushiriki kikamilifu katika sekta ya michezo.
Sambamba na hayo amewataka kufuatilia na kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Muwezeshaji wa mafunzo hayo Bi Hawra Shamte amesema usawa wa kijinsia unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mila na tamaduni, ubaguzi wa kisheria, ukosefu wa elimu, fikra na dhana potofu ya kijinsia, uchumi na ajira mambo ambayo yanakwamisha wanawake kushiriki katika michezo.
Amesema wanawake wanahaki ya kushiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa kikapu, ngumi na mpira wa miguu pekee bila kuathiri Mila,desturi na tamaduni zao.
Hivyo jamii , pamoja na wadau wanapaswa kuunga mkono michezo Kwa kuzingatia jinsia ili wanawake na wao waweze kupoga hatua za maendeleo kupitia michezo.
“Tofauti za kimaumbile zinaonekana kikwazo katika michezo ingawaje kuna baadhi ya wanawake wanafanya vizuri zaidi kuliko wanaume katika michezo, umefika wakati sasa WA Wanawake kushiriki michezo Kwa maendeleo.” mwezeshaji huyo.
Nao baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki katika mafunzo hayo wameahidi kuyafanyia kazi na kuleta mabadiliko katika jamii juu ya suala zima la ushiriki wa Wanawake katika michezo na maendeleo.
Mradi wa maendeleo ya Michezo Afrika "SPORTS DEVELOPMENT AFRICA, EMPOWERING GIRLS THROUGH SPORTS IN ZANZIBAR” una lengo la kuwawezesha wanawake na wasichana kupitia michezo unaendeshwa Kwa mashirikiano kati ya TAMWA ZNZ, Chama cha wanasheria wanawake (ZAFELA), chini ya ufadhili wa shirika la michezo la Ujerumani (GIZ).
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake