Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuzindua Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya Mwaka 2024 katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 5, 2024 jijini Dodoma.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Mei 27, 2024 kuhusu maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo amesema miongozo hii imelenga kuhakikisha kuwa Taifa linanufaika rasilimali za uchumi wa buluu.
Katika siku hiyo, Dkt. Jafo amefafanua kuwa Makamu wa Rais pia atagawa vyeti vya kutambua kampuni zilizoidhinishwa kuanza utekelezaji wa miradi ya kaboni pamoja na kukabidhi hundi kwa Halmashauri ya Katavi pamoja na kutambua mchango wadau katika kushiriki utunzaji na uhifadhi wa Mazingira.
Kwa mujibu wa Dkt. Jafo, katika wiki hiyo hiyo ya mazingira, pia kutakuwa na Kongamano la Kitaifa la wadau wa Mazingira ambalo litakuwa na kaulimbiu isemayo “Mabadiliko ya Tabianchi na Athari zake” litakalofanyika Mei 31, 2024 jijini Dar es Salaam.
Amesema kongamano hilo ambalo mgeni Mheshimiwa Makamu wa Rais limeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), litafanyika Katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
“Wadau watakaojumuika katika kongamano hilo ni pamoja na wataalam wa mazingira na sekta nyingine shirikishi kutoka Wizara na Taasisi za Serikali; Mashirika ya Kimataifa; Asasi za Kiraia; Sekta Binafsi; Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti. Wadau hao watapata fursa ya kujadili mada adhimu zinazohusu changamoto za hifadhi ya mazingira na kutoa mwelekeo na hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa na taifa letu,” amesema.
Halikadhalika katika kuchaguza wiki ya mazingira, Dkt. Jafo anatarajiwa kuzindua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa chini ya Mradi wa Urejeshaji wa Uoto wa Asili unaotekelezwa katika mikao mbalimbali nchini mikoa hiyo ni Mkoa wa Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi Mei 29, 2024.
Wiki ya Mazingira itaendea sambamba na Kampeni ya Usafi wa Mazingira Kitaifa, ambayo itafanyika katika maeneo mbalimbali ambayo ni Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam), eneo la Coco Beach, ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais. Dkt. Mpango, Kanda ya Ziwa (Mwanza) eneo la Soko la Samaki Mgeni Rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Magharibi (Kigoma), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Kusini (Lindi) usafi eneo korofi na , Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Lindi na usafi katika Mikoa - Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.
Vilevile amesema kutakuwa na Maonesho ya Wiki wa Mazingira ambapo wadau mbalimbali watapata fursa ya kuonesha bidhaa, teknolojia, uvumbuzi na ubunifu wa masuala mbalimbali yanayohusu hifadhi na uzimamizi wa mazingira.
Maonesho hayo yatafanyika katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Dodoma na kuzinduliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Dkt. Jafo ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika kuadhimisha maadhimhso haya kwa kushirikiana na Serikali katika shughuli hizi za maadhimisho.
No comments:
Post a Comment