ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 30, 2024

MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA MHE. HEMED SULEIMAN AFUNGUA MAFUNZO MAALUM


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu, Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wajumbe wa Sekretarieti ngazi za Matawi, Wadi na Majimbo katika Mafunzo Maalum ya kuwajengea uwezo wajumbe hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani , Mkoa wa Kusini Pemba.
Mjumbe wa kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa Ndugu.Hemed Suleiman amewataka wajumbe wa Sekretarieti ngazi za Matawi, Wadi na Majimbo kuwa mabalozi wazuri wa kuifikisha elimu waliyopatiwa kwa wanachama wenzao wa CCM ili kuendelea kukipa ushindi chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Akifungua mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Sekretarieti za CCM katika Ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Hemed amesema suala la kuwapatia mafunzo viongozi na wanachama wa CCM ni jambo zuri ambalo litawapelekea kuwa na uwelewa juu ya haki zao za msingi ikiwemo ile ya kupiga kura kwa kila mwanachama aliekidhi vigezo vya kupiga kura.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM amesema kuwa mafuzo ya wanayopatiwa wajumbe wa sekeretariet ya chama hicho yanamchango mkubwa sana wa kukisaidia chama kuendelea kushika hatamu awamu kwa awamu hivyo ni lazima viongozi wanaopatiwa mafunzo hayo kushuka chini kwa wafuasi wao ili kuweza kuwaelimisha juu ya mustakabali mzima wa chama.

Aidha Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ambae pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amesema ili Chama cha Mapinduzi kiendelee kushikilia dola ni lazima viongozi wawe na umoja, upendo na mshikamano pamoja na kufuata katiba, kanuni na Misingi ya chama cha Mapinduzi.

Amewataka viongozi kusimamia nidhamu ndani ya chama kwa kuwawajibisha wale wote watakaokiuka kanuni na taratibu za chama ili kuendelea kudumisha nidhamu ya uwajibikaji ndani ya CCM na kuweza kufikia malengo yaliyowekwa kupitia katiba ya chama cha Mapinduzi ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Aidha ndugu Hemed amewataka wanachama wa CCM kuendelea kukitumikia chama kwa uadilifu, haki na usawa sambamba na kuachana na harakati za kupanga wagombea na kupigiana kampeni kwa sasa na badala yake wawape muda viongozi waliopo madarakani kuwatumikia wananchi wao.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati Maalum Idara ya Oganaizesheni Ndugu. OMAR IBRAHIM KILUPI amesema viongozi ndio Jeshi la kukiletea Chama Cha Mapinduzi ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2020-2025, hivyo wanawajibu wa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano kwa maslahi mapana ya chama na Taifa kwa ujumla.

KILUPI amesema kuwa kila mwanachama wa CCM ana wajibu wa kuhakikisha anakilinda na kukitetea chama cha Mapinduzi na kujiepusha kuwa chanzo cha migogoro na mifarakano ndani ya chama siku hadi siku.

Akitoa maada katika mafunzo hayo ndugu KHADIJA NASSOR ABDI kutoka Idara ya Uenezi na Mafunzo ya CCM Zanzibar amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wajumbe wa Sekretarieti za CCM ngazi mbali mbali ili waweze kuwa viongozi wenye nidhamu, wawajibikaji na wenye kutunza siri za chama.

Amesema kiongozi anatakiwa kuwa mfano nzuri kati jamii anayoiongoza kwa kutoa ushirkiano. Kuvumilia changamoto mbali mbali sambamba na kujitoa katika kukitumikia chama na wanachama wake kwa ujumla.

Mafunzo hayo ya siku moja yaloandaliwa na Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui ambayo yanalenga kuwaandaa viongozi kuwa na nidhamu na wawajibikaji kwa mujibu wa katiba na kanuni za Chama cha Mapinduzi.

No comments: