Saturday, August 24, 2024

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AWAKUMBUSHA WAZAZI NA WALEZI KUHAKIKISHA WANAWASIMAMIA VYEMA VIJANA WAO


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ameendelea kuwakumbusha Wazazi na walezi kuhakikisha wanawasimamia vyema vijana wao katika kufuata maadili ya kiislamu kama ilivyoamrishwa katika kitabu kitukufu cha Qur-an.

Alhajj Hemed ameyasema hayo alipokuwa akiwasalimia Waumini wa Masjid Almarhum Mohammed Bindhahir uliopo Bububu Skuli mara baada ya kumaliza Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema uislamu umemtaka kila muumini kuhakikisha kuwa anamsimamia kila anaemuongoza kwa kumfundisha mema na kumkataza maovu yanayokwenda kinyume na maadili ya kiislamu yanayomuuongoza katika kila jambo likiwemo suala zima la kufanya ibada.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema jitihada za maksudi zinahitajika kwa wazazi na walezi kujitolea kuwapigania watoto wao na wale ambao wanawategemea katika mambo ya kheri kama kitabu kitukufu cha Qur- an kinavyoelekeza.

Alhajj Hemed amesema kuwa ni lazima wazazi na walezi kuhakikisha wanaimarisha umoja, upendo na mshikamano ili kuondoa yale yote ambayo hayaendani na maadili ya kiislamu katika jamii zao.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewataka wananchi wa Zanzibar na waumini wa dini ya kiislamu kuendelea kuitunza neema ya Amani na utulivu uliopo nchini ili kuweza kuisaidia Serikali kutekeleza yale yote ambayo imekusudia ya kimaendeleo kwa waanchi wake pamoja na kuwaachia vizazi vijavyo nchi yenye neema na mafanikio mengi.

Mapema akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Ustadh Twalib Abdalla Twalib amewataka waumini wa dini ya Kiislam na Wazanzibari kwa ujumla kuhakikisha wanatumia Maneno mazuri katika maisha yao ya kila siku ili kudumisha upendo baina yao.

Amesema kuwa uislamu umeweka utaratibu maalum wa kuzungumza baina yao na kuwalea watoto wao katika maadili na mafundisho mema ili kufuata nyayo za Mtume Muhammad ( S.A.W ) pamoja na kupata ujira ulio mwema hapa duniani na kesho akhera.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake