ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 2, 2024

RAIS DK.MWINYI KUFUNGUA TAMASHA FAHARI YA ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi anatarajia kufungua Tamasha la Fahari ya Zanzibar 2024 linalotarajia kufanyika Septemba 20 hadi 27 mwaka huu viwanja vya Nyamazi,Unguja.


Huku nchi sita zinatarajia kushiriki tamasha hilo kwa lengo la kujadili masoko na uwekezaji ambapo kutakuwa na Kongamano maalum ndani ya Tamasha hilo.

Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi,(ZEEA),Juma Burhan Mohamed wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya uwepo wa Tamasha la wiki moja la wajasiriamali "Fahari ya Zanzibar 2024" ambalo litakuwa chini ya Wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (ZEEA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania(TANTRADE).
Amesema tamasha hilo litahusisha vipengele vitatu muhimu ikiwemo kutoa fursa kwa wajasiriamali kuonesha na kuuza bidhaa na huduma zao pamoja kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kutoka taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.

"ZEEA na TANTRADE tulisaini hati ya makubaliano ya kushirikiana katika kuwawezesha wajasiriamali kupata masoko ya bidhaa na huduma zao ndani na nje ya nchi,"amesema na kuongeza

"Tamasha hili litakuwa na kauli mbiu "Fahari ya Zanzibar Kuimarisha Uwezeshaji Kidigitali "kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa matumizi ya kidijitali katika biashara,"amesema Mohamed.

Amesema miongoni mwa malengo la tamasha hilo ni pamoja na Kusaidia wajasiriamali wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupata masoko ya bidhaa na huduma zao,kuwaunganisha wajasiriamali wa Zanzibar na Tanzania Bara ili kushirikiana kukabiliana na changamoto, Kuwaunganisha wajasiriamali na taasisi za fedha kwa usaidiazi wa kifedha na Kukuza matumizi ya Kidijitali katika sekta ya masoko na Kutangaza huduma zinaotolewa na ZEEA.

Ameongeza kuwa tamasha hilo ni la pili kufanyika hivyo linatarajiwa kuwa kubwa zaidi kwa kushirikisha washiriki 1500 ambapo watashiriki tamasha hilo."Mwaka jana tamasha lilihusisha wanufaika wa huduma za ZEEA pekee,mwaka huu litahusisha wanufaika pamoja na washiriki wengine kutoka ndani na nje ya Tanzania, "amesema.

Pia ametoa shukrani na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa jitihada zao za kuleta maendeleo nchini.

Tamasha hilo litatarajiwa kufungwa na Waziri wa Nchi Kazi,Uchumi na Uwekezaji Sharif Ali Sharif Septemba 27 mwaka huu.



No comments: