Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi, akichangia mjadala kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean, na Pacific (OACPS) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 9 Agosti 2024
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America (DEA) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swaiba Mndeme akifuatilia Mkutano OACPS uliokuwa ukiendelea kwa njia ya mtandao.
Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi, akimwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.).
Mkutano huo, ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. TÉTE António, uliangazia masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Jumuiya, ikiwa ni pamoja na taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya mikutano iliyopita, maendeleo ya programu na miradi mbalimbali, hali ya kifedha ya Jumuiya, na maandalizi ya mkutano ujao wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa OACPS.
Katika hotuba ya ufunguzi, Mhe. António alisisitiza umuhimu wa mkutano huo katika kutatua changamoto mbalimbali, hususan za kifedha na kiutendaji, ili kuimarisha ufanisi wa Jumuiya.
Balozi Mbundi, akichangia katika mjadala, alisisitiza umuhimu wa matumizi bora ya rasilimali fedha na kuhimiza Sekretariati ya OACPS kuzingatia miongozo ya matumizi sahihi ya fedha ili kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa bajeti. Pia aliungana na wajumbe wengine kuhimiza nchi wanachama kumalizia michango yao kwa Sekretariati na kupunguza matumizi yasiyo ya maendeleo kama njia ya kukabiliana na upungufu wa fedha.
Balozi Mbundi alieleza kuwa hatua hizo zitasaidia kuimarisha imani ya nchi wanachama na wadau wa maendeleo ambao wanachangia kwenye bajeti ya miradi na programu mbalimbali za Jumuiya hiyo.
Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania ulijumuisha wawakilishi kutoka Wizara ya Fedha na Ofisi ya Makamu wa Rais, ukiongozwa na Balozi Stephen Mbundi.
No comments:
Post a Comment