ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 9, 2024

MAKAMU WA PILI WA RAIS AZINDUA MFUMK WA TAARIFA ZA ELIMU MASKULINI


Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abulla akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika hafla ya Uzinduzi wa Mfumo wa Taarifa za Elimu maskulini (School Information System- SIS) Uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Jijini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe, Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwepo kwa Mfumo wa Taarifa za Elimu maskulini (School Information System- SIS) kunalenga kuimarisha upatikanaji wa Takwimu kwa usahihi na kwa wakati uliopangwa.

Ameyasema hayo katika hafla ya Uzinduzi wa Mfumo wa Taarifa za Elimu maskulini (School Information System- SIS) katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Jijini Zanzibar.

Amesema kuwa kuwepo kwa mfumo wa Taarifa za Elimu maskulini ni nguzo muhimu katika kuyafikia malengo ya mageuzi ya Elimu nchini, ambao utawezesha kazi ya ukusanyaji, uchambuzi, uhifadhi na matumizi ya Takwimu kufanyika kwa urahisi na kwa ufanisi mkubwa kwa kupunguza gharama zilizokuwa zikitumiaka kabla ya Mfumo.

Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali imechukua hatua ya kuweka miundumbinu ya kisasa na kununua vifaa vya kidijitali vitakavyotumika katika mfumo huo ili uweze kufanya kazi kwa ubora uliokusudiwa.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais amesema malengo ya Serikali ni kuona Mfumo wa Taarifa za Elimu unatumika katika skuli za Serikali na Skuli binafsi ili kuhakikisha adhma ya Serikali ya kwamba ifikapo mwaka 2025 wanafunzi wote Zanzibar wanaingia kwa mkondo mmoja wa masomo inatimia pamoja na kufuta Divisheni zero katika ufaulu wa mitihani ya Taifa.

Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali imeanza mchakato wa kuziunganisha skuli na Mkonga wa Taifa ili ziweze kupata huduma ya Intaneti ya uhakika hatua itakayochochea kasi na ubora wa matumizi ya mfumo huo.

Mhe. Hemed ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuwasimamia walimu pamoja na Afisi za Elimu Mikoa na Wilaya kuhakikisha Taarifa zote zinazohitajika kujazwa ndani ya mfumo huo zinajazwa kikamilifu na kutumwa kwa wakati ili kufikia lengo la kuwepo mfumo huo.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Wizara ya elimu inatoa elimu kwa kutumia mifumo ya kidijitali hivyo ni wajibu wa walimu na wahusika wote kuutumia mfumo huo ambao Serikali imewekeza fedha nyingi katika utengenezaji wake.

Mhe. Lela amesema USAID na UNICEF kwa kushirikiana na uongozi wa Wizara ya Elimu wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanawajengea wanafunzi Msingi Madhubuti wa kusoma kupitia program zao mbali mbali zilizotoa hamasa ya kuanzishwa mfumo wa Taarifa za Elimu ambao utaboresha na kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya elimu Zanzibar.

Waziri Lela amesema Wizara ya Elimu itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na washirika mbali mbali wa maendeleo katika kufanikisha malengo ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa Zanzibar .

kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa linalosaidia watoto Duniani (UNICEF ) Dkt. Massoud Mohd Salim amesema Mfumo wa Taarifa za Elimu utasaidia kuimarisha upatikanaji wa taarifa na takwimu kwa ufasaha zaidi.

Dkt. Massoud amefahamisha kuwa ili Mfumo huo uweze kufanya kazi vizuri kunahitajika mashirikiano ya hali ya juu kati ya Wizara ya Elimu, walimu, wazazi na wadau wa elimu nchini katika kufikia mageuzi ya elimu Zanzibar na kuwa na mifumo Imara ya Kufundishia na kusomea.

Akiwasilisha taarifa ya Mfumo wa Taarifa za Elimu Naibu Katibu Mkuu Utawala kutoka Wizara ya Elimu Khalid Waziri amesema Mfumo wa Taarifa za Elimu utasaidia katika ukaguzi, uandaaji wa mitihani na uchakataji wa taarifa za walimu na wanafunzi waliotoroka skuli ili kila mtoto aweze kupata haki yake ya msingi ya kusoma.

Khalid amesema walimu wa ngazi zote kuanzia maandalizi hadi Sekondari wameshapatiwa mafunzo ya awali na tayari wanafunzi wameshaanza kusajiliwa katika mfumo huo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe 09 / 10 / 2024.

No comments: