Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Wizara ya Afya, watendaji wa kada ya Ganzi na Usingizi, wanafunzi wa Afya na wananchi waliohudhuria katika Maadhimisho ya siku ya wataalamu wa Ganzi na Usingizi duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuhakikisha wataalamu wa ganzi na usingizi wanawekewa mazingira bora ya utendaji wa kazi zao ili kuendelea kufanyika upasuaji salama katika hospital zote nchini.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla katika Maadhimisho ya siku ya wataalamu wa Gansi na Usingizi duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.
Amesema Taaluma ya Ganzi na usingizi ni miongoni mwa Taaluma muhimu katika kada ya Afya hivyo Serikali itahakikisha inawawekea mazingira bora wataalmu hao ikowemo kuwapatia maslahi na stahiki zao zote pamoja na fursa za masomo ya ndani na nje ya nchi ili kuwaongezea ari ya utendaji wa kazi zao.
Mhe.Hemed amesema kuboreshwa na kuimarishwa kwa Sekta ya Afya nchini hususan katika kada ya Ganzi na Usingizi kutarejesha hadhi na heshima ya kada hio na kutawavutia vijana wengi zaidi kuipenda fani ya Ganzi na Usingizi ambao watasaidia kutoa huduma hio katika Hospitali mbali mbali nchini.
Aidha, Makamu wa Pili wa Rais ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya kukaa pamoja na wataalamu wa Ganzi na Usingizi ili kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili kada hio ikiwemo kununua vifaa vya kisasa, kupatiwa haki na stahiki zao pamoja kupatiwa mafunzo yatakayo wakumbusha wajibu wao wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi.
Mhe. Hemed amesema wakati umefika kwa Wizara ya Afya kushirikiana na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuanzisha kada ya Ganzi na Usingizi ambayo imekuwa na uhitaji mkubwa wa Wataalamu hapa visiwani.
Sambamba na hayo Mhe.Hemed amewataka wataalamu wa Afya kuendelea kutoa huduma kwa kufuata maadili ya kazi zao ikiwemo upendo, huruma na moyo wa kujitolea kwa wagonjwa, na kutoa wito kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya diploma ya uuguzi kuwa tayari kujiunga na kada hio ili kuweza kuwa na wataalamu wengi katika maeneo ya kiutolea huduma.
Nae Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazurui amesema Wizara imejipanga kuimarisha na kuiboresha Taaluma ya Ganzi na Usingizi kwa kuwasomesha na kuwaendeleza kitelimu watendaji wa kada hio pamoja na kununua vifaa vya kisasa vitakavyorahisisha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Mazurui amesema kada ya Ganzi na Usingizi imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa na madaktari wasaidizi pamoja na uhaba wa vifaa tiba vya kisasa ambapo kwa Zanzibar nzima madakatari bingwa wa Ganzi na usingizi ni wanne(4) tu ambao hawatoshelezi kulingana na uhitaji wa tiba hio.
Amewataka wanafunzi wanaojiunga na vyuo kuchagua kozi kulingana na soko la ajira na uhitaji wa wataalamu ikiwemo kada ya Ganzi na Usingizi jambo litakalosaidia kupata wataalamu walio wengi na wabobezi wa kada hio.
Waziri Mazurui ameiomba Serikali na wamiliki wa vyuo binafsi nchini kuanzisha kozi ya Ganzi na Usingizi katika vyuo vyao ili kupanua wigo zaidi wa wanafunzi kujisome kada hio sambamba na kuzalisha watalaamu wazawa na wazelendo wa fani hio.
Akisoma Risala katika maadhimisho hayo mtaalamu wa ganzi na usingizi DKT. SABRINA ABDALLA ALI amesema kada ya Usingizi na Ganzi imekosa kutambulika rasmi kama kada nyengine kutokana na kukosa usimamizi madhubuti na mfumo rasmi wa utendaji wa kazi.
Ameiomba Wizara ya Afya kuiangalia kwa umakini na umuhimu wa kipekee kada ya ganzi na usingizi kwa kutoa kipaombele hasa katika kuwaendeleza kimasomo watendaji wa kada hio pamoja na kuwashawishi wanafunzi kusomea kada ya ganzi na usingizi kwa maslahi ya taifa.
Mapema Makamu wa pili wa Rais ametembelea mabanda ya maonesho na kuona kazi mbali mbali za kitaalamu zinazofanywa na madaktari hao.
Imetolewa na kitengo cha Habari ( OMPR)
No comments:
Post a Comment